Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, Alhamisi aliwataka wadau wote nchini Somalia kuwa na busara na utulivu na kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha ongezeko la vurugu kufuatia taarifa za machafuko katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
"Katibu Mkuu amesikitishwa na taarifa za vurugu huko Mogadishu," alisema msemaji wake, Stephane Dujarric, katika taarifa.
Dujarric alisema kuwa Guterres alisisitiza “umuhimu wa haraka wa wadau wote kurejea mezani kwa mazungumzo ili kutafuta suluhu na kuepuka na hatua zitakazorudisha nyuma maendeleo ambayo Somalia imepata hadi sasa, pamoja na kuhakikisha ulinzi wa raia na miundombinu ya kiraia.”
"Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande zote kuwa watulivu, kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuchochea vurugu zaidi, na kutatua tofauti za kisiasa kupitia mazungumzo," taarifa hiyo iliongeza.
Taarifa hiyo pia ilinukuu onyo kutoka kwa Misheni ya Umoja wa Mataifa ya kutoa Msaada Nchini Somalia (UNTMIS), ambayo imesema kwamba misheni hio pamoja na washirika wa kimataifa wamekuwa wakionya mara kwa mara kuhusu hatari ya kurejea kwa mgogoro wa kisiasa.
UNTMIS ilisema kwamba onyo lao halikuzingatiwa.
"Misheni ya Umoja wa Mataifa inawasihi viongozi wote wa Somalia kuweka mbele maslahi ya taifa na kurejea kwenye mazungumzo yaliyositishwa tarehe 15 Mei. Washirika wa kimataifa wa Somalia wako tayari kusaidia kufanikisha mazungumzo hayo," ilisema taarifa hiyo.

























