Wafanyakazi kutoka wizara mbalimbali, pamoja na taasisi za umma na binafsi wamejitokeza katika maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo inafanyika Mei Mosi ya kila mwaka.
Nchini Kenya, Rais William Ruto ameongoza maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Kaunti ya Vihiga, magharibi mwa nchi.
Wakati akiwahutubia wafanyakazi waliohudhuria maadhimisho hayo na wale waliokuwa wakifuatia kupitia mitandao ya kijamii, Rais Ruto ametangaza nyongeza ya asilimia 12 ya mshahara kwa wafanyakazi na nyongeza ya asilimia 15 ya mishahara katika sekta ya kilimo.
Awali Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi nchini Kenya Francis Atwoli aliomba nyongeza ya asilimia 23.
Rais Ruto alibainisha kuwa agizo hilo lililenga zaidi kuboresha ustawi wa wafanyakazi wakati ambapo kumeshuhudiwa kupanda kwa gharama za maisha.
Rais Ruto alimaliza hotuba yake kwa kuwatakia Wakenya heri ya Siku ya Wafanyakazi kwa kusema, "Kwa wafanyakazi wote wa Kenya, nawatakia heri ya Siku ya Wafanyakazi. Naomba tuendelee kujenga taifa hili pamoja kwa ajili ya kizazi hiki na kijacho, tunapojitahidi kubadilisha Kenya kuwa uchumi uliostawi katika maisha yetu."
Rais Museveni ahimiza kilimo
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amewataka raia wake kuwekeza zaidi katika kilimo ili kutengeza nafasi zaidi za ajira.
Museveni amesema Uganda ina ekari zipatazo milioni 40 za ardhi inayofaa kwa kilimo na ni milioni 7 tu ndizo zinazotumika ipasavyo, huku kila ekari ikitoa ajira kwa watu 15 kazi. Amesema hiyo, ni sawa na kuwa na takriban ajira milioni 105 kwa jumla ambazo ni zaidi ya idadi ya watu wa nchi hiyo.
Rais Museveni alisema hayo alipokuwa akiongoza taifa wakati wa sherehe za siku ya Wafanyakazi zilizofanyika wilayani Buikwe, eneo la Kati nchini Uganda.
Rais wa Burundi aangazia umuhimu wa wafanyakazi
Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye aliongoza wafanyakazi katika sekta mbalimbali katika kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani.
Rais Ndayishimiye amesifu mchango wa wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali na kusema kuwa wao ndio uti wa mgongo wa uchumi.
Sherehe hizo zilifanyika Gitega, mojawapo ya miji ya Burundi.
Nayo nchini Tanzania, Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan aliongoza maelfu wa wananchi waliojitokeza katika maadhimisho hayo ambayo kitaifa, yamefanyika Mkoani Njombe.
Sherehe za mwaka huu zinafanyika huku kilio kikubwa cha wafanyakazi kikiwa ni kupanda kwa gharama za maisha. Hali hii imechangiwa zaidi na mgogoro wa Mashariki ya Kati ambapo mbali na kushuhudiwa kwa uhaba wa mafuta, lakini pia mgogoro huo umechangia kwa kiasi kikubwa kupanda kwa bei za bidhaa muhimu kama chakula na usafiri.











