Balozi wa Uturuki mjini Damascus, Nuh Yilmaz, alisema kuwa vitisho vikuu vya kiusalama kwenye mpaka wa Uturuki na Syria vimetoweka tangu utawala mpya wa Syria ulipoingia madarakani.
Yilmaz alizungumzia uhusiano wa kidiplomasia kati ya Ankara na Damascus pamoja na hali ya mambo katika eneo hilo, katika mahojiano na kipindi cha "Syria Now" cha kituo cha televisheni cha Al Jazeera chenye makao yake makuu nchini Qatar.
Alisema kuwa ujumbe mkubwa zaidi wa kidiplomasia wa Uturuki duniani upo Damascus, akisisitiza mizizi ya kihistoria ya uhusiano wa nchi hizo mbili, pamoja na ushirikiano wa kijeshi na kiuchumi na azma ya pamoja ya kupambana na ugaidi.
Akigusia uhusiano wa kina wa kihistoria na kiutamaduni kati ya Uturuki na Syria, Yilmaz alisema kuwa Damascus ina nafasi ya kipekee katika kumbukumbu ya taifa la Uturuki.
"Katika historia yote, mji huu wa kale, unaojulikana kama 'Sham al-Sharif,' umebeba urithi wa kina unaoanzia Dola ya Ottoman hadi Seljuk.
"Kuanzia wito wa kusali katika Msikiti wa Umayyad hadi mila zetu za pamoja, alama bainifu zaidi za utamaduni wetu zinaendelea kuwepo hapa," alisema.
‘Matatizo ya kiusalama yametoweka’
Akichambua hali ya usalama na mawasiliano ya kijeshi kati ya nchi hizo mbili, Yilmaz alirejelea msimamo wa Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, kwamba "usalama wa Syria ni usalama wa Uturuki."
Alisema kuwa matatizo makuu ya kimkakati ya kiusalama kwenye mpaka huo yametoweka kufuatia mabadiliko ya utawala nchini Syria.
"Baada ya tarehe 8 Desemba 2024, matatizo manne ya kimkakati ya kiusalama — usafirishaji haramu wa binadamu, biashara ya dawa za kulevya, uhamiaji usiodhibitiwa na ugaidi — yalitoweka ghafla kwenye mpaka wetu," alisema Yilmaz.
Pia alitaja ziara ya meli za jeshi la wanamaji la Uturuki katika Bandari ya Latakia kama ishara thabiti ya ushirikiano wa kijeshi na wa masuala ya bahari katika siku zijazo.
"Ziara ya meli za jeshi la wanamaji la Uturuki katika Bandari ya Latakia pia ni ishara thabiti zaidi ya ushirikiano tutakaofanya katika nyanja za kijeshi na masuala ya bahari katika kipindi kijacho.
"Tuko tayari kusimama pamoja na jeshi la Syria katika kukidhi mahitaji yake ya mafunzo, vifaa na usafirishaji na ugavi (logistics)," alisema.
Ankara inafuatilia mchakato huo kwa karibu
Yilmaz alisema msimamo wa Uturuki kuhusu makundi ya kigaidi katika eneo hilo ulikuwa wazi, akisisitiza kuwa ni lazima PKK/YPG/SDF ziondolewe kabisa kutoka eneo hilo.
Alisema Ankara inafuatilia kwa karibu mchakato kati ya serikali ya Syria na YPG, akiongeza kuwa kuondolewa kabisa kwa makundi ya PKK na SDF kote Uturuki, Syria, na Iraq ni muhimu ili kulinda mamlaka na ukamilifu wa eneo la ardhi ya Syria.
"Tunatazamia ndoto ambayo si tu ya mazingira ambapo ugaidi umekoma nchini Uturuki, bali katika eneo letu lote.
"Kuondolewa kabisa kwa makundi ya SDF na PKK kote Uturuki, Syria, na Iraq ni muhimu kwa ajili ya mamlaka na ukamilifu wa eneo la ardhi ya Syria.
"Kama Rais (wa Syria) Ahmed al-Sharaa alivyosema pia, ingawa mchakato wa ujumuishaji unaendelea polepole, tunaunga mkono hatua zinazolenga kukomesha ugaidi," alisema Yilmaz.
Lengo la kufikia biashara ya dola bilioni 10
Kuhusu uhusiano wa kiuchumi, Yilmaz alisema kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili kiliongezeka kwa asilimia 40 katika kipindi kifupi na kufikia dola bilioni 3.75, huku lengo la muda wa kati likiwa ni kufikia dola bilioni 10.
Alisema mazungumzo yanaendelea kuhusu makubaliano ya biashara huria na maeneo ya pamoja ya viwanda.
Kuhusu vituo vya mpakani, alisema Uturuki inalenga kufungua tena vituo vyote kwenye mpaka huo wenye urefu wa zaidi ya kilomita 900 (maili 559).
"Tunalenga kufungua vituo vyote kwenye mpaka wetu, ambao una urefu wa zaidi ya kilomita 900. Chini ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya Wizara yetu ya Biashara na mamlaka za forodha za Syria, tunatarajia vituo vya mpakani, hasa kwenye njia ya Nusaybin-Qamishli, kuanza kufanya kazi hatua kwa hatua ndani ya miezi mitatu.
"Aidha, mradi wa Eneo Huru la Biashara na Bandari Kavu utakaowekwa Idlib utaharakisha taratibu za usafirishaji na forodha," alisema.
Yilmaz pia alisisitiza umuhimu wa kusaidia sekta ya elimu nchini Syria. Alisema kuwa, chini ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya Wizara ya Elimu ya Taifa ya Uturuki na mamlaka za Syria, shule ya kimataifa ya Uturuki itafunguliwa mjini Damascus na maeneo ya jirani katika kipindi kijacho.
Kuhusu raia wa Syria walio chini ya mpango wa ulinzi wa muda nchini Uturuki, Yilmaz alisema kuwa tayari kulikuwa na utaratibu wa kuwapa msamaha dhidi ya masharti ya vibali vya kazi kwa muda mrefu sasa.
Aliongeza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uturuki zinafanyia kazi taratibu mpya za visa ili kurahisisha ziara za kwenda Uturuki kwa raia wa Syria wanaorejea nchini mwao.
Ziara ya Erdogan mjini Damascus
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa Rais Erdogan kufanya ziara nchini Syria, Yilmaz alisema kuwa safari hiyo bado ni jambo linalotarajiwa na kutamaniwa.
"Rais ana mapenzi makubwa kwa Damascus na Msikiti wa Umayyad. Mawasiliano yaliyokuwa yamepangwa awali yaliakhirishwa kutokana na matukio yaliyojitokeza katika eneo hilo.
"Tunatumai kumuona Rais akiwa Damascus kabla ya mwisho wa mwaka huu. Picha ile ya kihistoria ya Rais Erdogan na Bw. al-Sharaa wakitembea pamoja katika Msikiti wa Umayyad ingedhihirishia dunia nguvu ya ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili," alisema.






















