Ni Seneta wa Kaunti ya Nairobi, ambao ndiyo mji mkuu wa Kenya. Amezaliwa magharibi mwa nchi hiyo na umri wake ni miaka 44. Mwanasiasa huyu kitaaluma ni mwanasheria ambapo shahada yake alipata katika Chuo Kikuu cha Nairobi mwaka 2006.
Edwin Sifuna alijijengea jina kama mwanasiasa jasiri, mwenye ari na uwezo mkubwa wa kuwasilisha hoja.
Safari yake ya kisiasa na kuimarika kwake kulihusishwa zaidi kwa karibu na chama cha ODM na hasa kiongozi wa chama hicho wakati huo Raila Odinga.
Mwaka 2018, aliteuliwa rasmi kuwa Katibu Mkuu wa chama kikubwa cha upinzani ODM.
Akiwa Katibu Mkuu, Sifuna alionekana kuwa mmoja wa sauti zenye hamasa katika chama, na hili huenda lilimpa nafasi nzuri ya kuchaguliwa Seneta wa Nairobi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2022.
Hata hivyo, kitumbua kiliingia mchanga wakati uhusiano wake na chama cha ODM ulipotatizika, na Februari 2026 akaondolewa katika nafasi ya Ukatibu Mkuu.
Sifuna akawa mmoja wa viongozi muhimu wa vuguvugu lilojulikana kama Linda Mwananchi, ambalo linahamasisha uwajibikaji, heshima kwa haki za mwananchi, na uongozi wenye uweleledi.
Leo, Sifuna anaendelea kujiimarisha kama kiongozi mbadala na mwenye tija kuelekea uchaguzi wa 2027.
Je, Sifuna ataendelea kuvuna au atabaki kuguna tu?
















