Nchi ya Senegal iliyo Afrika Magharibi, inaongozwa na Rais Bassirou Diomaye Faye ambae ana umri wa miaka 46.
Rais Faye ana wake wawili ambao ni Marie Khone Faye na Absa Faye.
Marie Khone Faye ndiye mke wa kwanza wa Rais Faye. Walifunga ndoa mwaka 2009.
Ana shahada ya uzamili ya mambo ya benki na bima.
Mwaka 2015 na 2016, Marie Khone alifanya kazi katika taasisi ndogo ya ufadhili.
Baada ya mume wake kuwa Rais mwaka 2024, Marie amechukua majukumu mengine ambayo ni pamoja na kuwa balozi wa kampeni ya "Zaidi ya Mama," ambapo anaendesha kampeni ya kuvunja unyanyapaa wa utasa, kuboresha uwezo wa huduma ya afya, na kuendeleza elimu ya wasichana.
Aprili 2026, alitangaza ujenzi wa "Maison des femmes" yani Nyumba ya Wanawake huko Ndiaganiao ili kusaidia wanawake wa eneo hilo.
Amekuwa pia sauti maarufu ya uwajibikaji wa mazingira, na mtetezi wa kupambana na uharibifu wa chakula.
Marie na mume wake, wamejaaliwa watoto wanne, wavulana watatu na msichana mmoja.
Mwaka 2023 Faye alimuoa Absa kama mke wa pili, mwaka mmoja tu kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Senegal.
Absa Faye amezaliwa mwaka 1993, nae ana shahada ya uzamili katika usimamizi.
Kabla ya kuchukua majukumu ya mke wa Rais, alifanya kazi katika sekta ya benki nchini Ufaransa na aliwahi kufanya kazi kama mratibu wa mradi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA).
Absa anashirikiana na mke mwenzake katika miradi mbalimbali ya kijamii.
Tangu mume wake aingie madarakani, amekuwa akifanya kazi katika nyadhifa rasmi, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono miradi ya mashirika ya misaada ya kibinadamu.
Walipata mtoto wao wa kwanza wa kike, Januari 2025.




















