Mataifa wanachama wa Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) wamepiga kura ya pamoja ya kususia Kombe la Dunia na mashindano mengine ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) yakipinga mpango wa FIFA wa kuuza hisa kwa wawekezaji ambao watasimamia michuano ya shirikisho hilo duniani, UEFA ilisema wakati wa kikao chake kwa njia ya video siku ya Alhamisi.
Siku ya Jumanne shirikisho hilo la soka duniani lilisema lina mpango wa kuunda shirika kwa gharama za dola bilioni 20 ambalo litasimamia Kombe la Dunia na mashindano mengine na kwamba lingeuza hadi asilimia 20 za hisa kwa wawekezaji.
"Hakuna timu yoyote ya taifa ya UEFA ambayo itashiriki mashindano ya FIFA kama mpango huo bado utaendelea kuwepo, hadi pale mapendekezo hayo yatakapotupiliwa kabisa na hakikisho kutolewa kuwa FIFA katu haitozungumzia mipango ya usimamizi au kutoa fursa ya usimamizi wa mashindano kwa kampuni binafsi," UEFA ilisema kwenye taarifa.
"Kombe la Dunia haliwezi kutumiwa kama sehemu ya uwekezaji. Ni moja ya urithi mkubwa wa mchezo wa soka. Msingi wake umejengwa kwa muda mrefu na vizazi mbalimbali vya wachezaji, timu za taifa, na mashabiki kutoka mabara yote," UEFA iliongeza.
"Sehemu yoyote ya urithi huo haitakiwi kuachiwa wawekezaji binafsi. Kombe la Dunia halitakiwi kuuzwa."


















