Mwenge wa Olimpiki ulipokelewa kwa muziki na ngoma katika mji mkuu wa Senegal siku ya Jumamosi, huku maandamano ya wanawake 100 yakiashiria kuanza kwa hesabu ya siku kuelekea tukio la kwanza la michezo ya Olimpiki kufanyika barani Afrika.
Mamia ya watu walikusanyika katika eneo la Place du Souvenir Africain jijini Dakar—uwanja wa wazi ulioko kando ya Bahari ya Atlantiki na kuzungukwa na picha za watu mashuhuri kutoka Afrika na jamii ya Waafrika waishio ughaibuni—ili kuupokea mwenge huo kabla ya Michezo ya Olimpiki ya Vijana itakayofanyika mwezi ujao.
Wanawake walioubeba mwenge huo wanajulikana kama "lingeer" — jina la heshima kwa malkia au wanawake wa kifalme katika lugha ya Wolof, mojawapo ya lugha kuu nchini Senegal.
'Afrika ina uwezo na haiwezi kuzuilika'
Wakiwa wamevalia mavazi ya asili yanayotiririka ya rangi ya chungwa na dhahabu pamoja na vitambaa vya kichwa vya rangi ya njano, waliupeleka mwenge huo kwenye uwanja huo katika maandamano ya kusherehekea wanawake wa Senegal na urithishaji wa tunu na maadili kati ya vizazi.
"Kwa mara ya kwanza katika historia yake, mwenge huu unawaka katika ardhi ya Afrika kwa ajili ya michezo iliyoandaliwa barani Afrika. Nilitaka kuupokea nikiwa katikati ya vijana, ambao walitoka katika vitongoji vyote vya Dakar. Mwenge huu ni mali yao, dunia imeichagua Senegal kwa ajili yao, na kupitia wao ndipo Michezo ya Olimpiki ya Vijana ya Dakar 2026 itakapofanikiwa," alisema Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, baada ya kuupokea mwenge huo.
Gwiji wa mpira wa kikapu kutoka Senegal, Mame Maty Mbengue, aliwasha mwenge wa Olimpiki katika hafla hiyo.
Kirsty Coventry, raia wa Zimbabwe na kiongozi katika Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, alisema tukio hilo litakuwa "wakati wa fahari" kwa Senegal na bara zima.
"Kila mtu atakayekuja Senegal katika wiki chache zijazo ataondoka akijua kuwa Afrika na Senegal zina uwezo na haziwezi kuzuilika, na kwamba kizazi chetu cha vijana kitabadilisha dunia," Coventry aliwaambia watu waliohudhuria.
Takriban wanariadha 2,700, michezo 35
Mwenge huo uliondoka katika mji mkuu wa Ugiriki, Athens, siku ya Alhamisi—ambapo uliwashwa kwa kutumia miale ya jua na kioo maalum (parabolic mirror) kulingana na desturi za Olimpiki—kabla ya kukabidhiwa kwa Senegal katika Uwanja wa Panathenaic.
Mwenge huo utaanza ziara ya kilomita 3,600 (maili 2,237) nchini Senegal siku ya Jumatatu, ukipita katika mikoa yote 14 huku zaidi ya Wabebaji mwenge 400 wa Senegal wakipokezana, kabla ya kurejea katika mji mkuu kwa ajili ya sherehe rasmi ya ufunguzi.
Michezo ya Olimpiki ya Vijana, itakayofanyika kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi 13 Novemba, itawakutanisha takriban wanariadha vijana 2,700 kushindana katika michezo 35 jijini Dakar na miji ya karibu ya Diamniadio na Saly.
Michezo ya Olimpiki ya Vijana, ambayo ilifanyika kwa mara ya kwanza nchini Singapore mwaka 2010, ni toleo dogo la Michezo ya Olimpiki lililokusudiwa wanariadha wenye umri wa miaka 15 hadi 18.



















