Chama cha soka cha Palestina (PFA) kimedai kuwa Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) lilishindwa kutumia baadhi ya sheria zake dhidi ya Israel kwa matendo yake yanayoendelea kuathiri ustawi wa mchezo wa soka nchini Palestina.
Katika taarifa yake ya Jumatatu, PFA ilidai kuwa zaidi ya watu 1000, wanaojihusisha na mchezo huo nchini Palestina, wameuawa katika eneo la Gaza, huku viwanja vya michezo na maeneo mengine yakiharibiwa vibaya.
Chama hicho, kimeikosoa FIFA kwa kuendelea kukaa kimya na kutochukua hatua dhidi ya vitendo vya Israel dhidi ya Palestina.
"Ukimya huu hauridhishi hata kidogo, hatuwezi kuendelea kusikiliza ahadi zisizotimizwa."
Mwaka jana, FIFA ilisema haitoifungia Israel kushiriki michezo ya kimataifa, kwani haihusiki na changamoto za kisiasa.
Mashabiki wa soka, wameikosoa FIFA kwa upendeleo, kwa kushindwa kuiadhibu Israel, wakati ilifanya hivyo kwa Urusi kufuatia vita vya Ukraine.
















