Raia wa Malawi wanaokusudia kusafiri kwenda Marekani sasa lazima waombe viza kutoka Kenya, kufuatia sera mpya ya Marekani.
Hatua hii inaashiria mabadiliko makubwa zaidi barani Afrika huku Washington ikianzisha mfumo mpya wa kushughulikia viza kuanzia tarehe 1 Agosti 2026.
Katika tangazo lililotolewa tarehe 15 Julai, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema itasitisha huduma za kawaida za viza katika miji mingi barani Afrika, na kuelekeza waombaji kwenye vituo vichache vilivyoteuliwa vya kikanda.
Kwa raia wa Malawi, kituo chao cha viza kitakuwa katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
Vituo vya kushughulikia viza vimefungwa
Si Malawi pekee iliyoathirika. Marekani imefunga vituo vyake vya kushughulikia viza katika miji 25 barani Afrika, ikiwemo Abuja nchini Nigeria, Asmara nchini Eritrea, Durban nchini Afrika Kusini, Harare nchini Zimbabwe, Juba nchini Sudan Kusini, Lusaka nchini Zambia, Ouagadougou nchini Burkina Faso, na Antananarivo nchini Madagascar.
Kwa vitendo, utaratibu huu unamaanisha kuwa waombaji viza lazima wasafiri kwenda nchi nyingine za Afrika au miji mingine iliyoteuliwa ndani ya nchi zao wenyewe.
Kwa raia wa Malawi, hali inaonekana kuwa ngumu zaidi.
Kuondolewa kwa huduma za viza jijini Lilongwe na kuhamishia kila kitu Nairobi, Kenya, kunaongeza mzigo mpya wa changamoto, kuanzia masuala ya nyaraka hadi gharama za usafiri.
Malawi iko kusini mwa Afrika huku Kenya ikiwa Afrika Mashariki. Umbali kati ya Lilongwe na Nairobi ni karibu kilomita 2,000. Safari hiyo huchukua takriban saa tatu kwa ndege na siku mbili hivi kwa barabara.
Dhamana za visa zinazoweza kurejeshwa
Hii ina maana kwamba raia wa Malawi lazima wavuke mipaka kadhaa ili kufika Nairobi kwa ajili ya mchakato wa viza ya Marekani iwapo watasafiri kwa barabara.
Ingawa raia wa Malawi hawahitaji viza ya kawaida kuingia Kenya, wanatakiwa kuomba mtandaoni Kibali cha Kusafiri kwa Njia ya Kielektroniki (eTA) kabla ya kusafiri.
Mchakato huo mpya pia unahusisha gharama za ziada za kifedha na muda, ikiwemo tiketi za ndege au nauli ya usafiri wa barabarani pamoja na gharama za malazi na chakula nchini Kenya.
Raia wa Malawi pia ni miongoni mwa Waafrika wanaotakiwa kulipa dhamana ya lazima ya viza inayoweza kurejeshwa, ambayo inaweza kufikia dola za Marekani 15,000.
Ajenda ya ‘Marekani Kwanza’
Na kama ilivyo kwa mwombaji yeyote kutoka mahali popote, kupata viza ya Marekani si jambo la uhakika. Maombi yanaweza kukataliwa hata baada ya kupitia usumbufu wote huo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema kuwa sera hiyo mpya ni sehemu ya ajenda ya utawala wa Trump ya "Marekani Kwanza," inayolenga kuimarisha usalama wa taifa, kupunguza gharama, na kuhakikisha kuwa "serikali inafanya kazi kwa maslahi ya wananchi wa Marekani."
Utawala wa Trump pia umetekeleza sera mbalimbali za uhamiaji duniani kote, ikiwemo marufuku ya kusafiri na mipango ya dhamana ya viza (inayohusisha hadi dola 15,000) ambayo huathiri zaidi nchi za Afrika.




















