Nairobi imeteuliwa kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Riadha ya Dunia 2029, huku mji mkuu huo ukiwa wa kwanza barani Afrika kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.
Shirikisho la Riadha Duniani limetangaza uamuzi huo siku ya Jumanne baada ya mkutano wa baraza lake jijini Budapest, huku jiji la Munich likipewa uwenyeji wa mwaka 2031.
Nairobi ilishindwa katika kuwania uwenyeji wa mwaka 2025, ambapo jiji la Tokyo lilipata nafasi hiyo. Mji mkuu wa Kenya umewahi kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Dunia ya U18 mwaka 2017 na Dunia U20 mwaka 2021.
Mashindano hayo yatafanyika katika Uwanja wa Kasarani, ambao unakarabatiwa kwa ajili ya mechi za AFCON 2027.
Mafanikio ya maombi
"Nairobi iliwasilisha ombi la kimkakati na la kuvutia, na kufanikiwa kuyapeleka Mashindano hayo ya Riadha ya Dunia barani Afrika kwa mara ya kwanza katika historia," alisema Rais wa Shirikisho la Riadha la Dunia Sebastian Coe.
"Kenya ni moja ya mataifa makubwa katika mchezo wa riadha. Mchezo huo ni sehemu ya utambulisho wa nchi hiyo."
Mji wa Munich utakuwa mwenyeji wa mchezo huo 2031 katika Uwanja wa Olimpiki, kufanikisha kurudisha michezo hiyo nchini Ujerumani kwa mara ya kwanza tangu Berlin mwaka 2009.
“Ujerumani imeonesha mara kwa mara kuwa ina uwezo wa kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya riadha,” Coe alisema.
Mashindano yote yatafanyika mwezi Septemba, kulingana na michezo ya 2027 jijini Beijing.




















