Macho na masikio, kwa sasa yapo kwa watu maarufu nchini Kenya, ambao wamehusishwa na matamshi ya chuki, mwaka mmoja kabla ya uchaguzi wa nchi hiyo.
Kauli na matamshi hayo, yanadaiwa kushika kasi katika siku za karibuni, huku taasisi ya Kofi Annan ikitahadharisha kutokea kwa machafuko, kwenye uchaguzi mkuu mwakani.
Haya yanajiri, wakati ambapo taifa hilo lina sheria zinazodhibiti matamshi hayo.
Hata hivyo, wachunguzi wa mambo, wadai kuwa, baadhi ya wanasiasa na watumiaji wa mitandao ya kijamii, wanatumia mbinu mbadala za kuepuka kuingia kwenye mtego huo.
“Hii ni ishara ya wazi ya namna siasa za Kenya zinavyoendeshwa,” anasema mtaalamu wa historia ya Kenya, Kenneth Ombongi, katika mahojiano yake na TRT Afrika.
Mapema mwezi huu, Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Maridhiano (NCIC), ilifungua jalada la madai dhidi ya Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Aden Duale, ambaye alidaiwa kufananisha moja ya jamii za nchi hiyo na mnyama aina ya fisi.
Kwa upande wake, waziri huyo, alitetea kauli zake, akasema kuwa hakueleweka na hatokuwa tayari kwenda mbele ya tume hiyo.
Kulingana na sheria za Kenya, waziri yeyote anayekabiliwa na makosa ya jinai, anapaswa kujiuzulu.
Wiki iliyopita, polisi wa nchi hiyo walimkamata mbunge wa Mukurwe-ini, John Kaguchia kwa kosa la kutoa kauli za chuki, na baadaye kuachiwa kwa dhamana.
Hata hivyo, kauli za chuki si kitu kipya nchini Kenya.
Kati ya mwaka 2007-08, vurugu baada ya uchaguzi zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200, na kuwaacha mamilioni wengine bila ya makazi.
“Tofauti zetu za kikabila zina nafasi kubwa sana katika siasa za nchi yetu, na mazingira haya hustawisha kauli za chuki,” anaongeza Ombongi.
“Ukiangala mazingira ya sasa, unaweza kuiona tofauti kidogo na ile ya 2007, hata hivyo matamshi ni yale yale,” anasema Ombongi.
Uhuru wa kutoa maoni dhidi ya kauli za chuki
Mapema mwezi huu, timu maalumu inayohusisha jeshi la polisi na watendaji kutoka tume ya uchaguzi, ilitahadharisha kuhusu mwenendo wa kauli za chuki nchini Kenya.
Kulingana na tume hiyo, mashauri zaidi ya 20, yalikuwa yakichunguzwa, kubaini viashiria vya kauli za chuki na za kichochezi.
Wale watakaopatikana na hatia, watanyimwa fursa za kuwania nafasi za kisiasa, hapo mwakani.
“Kila mtu ana haki na uhuru wa kutoa maoni yake, lakini ni vigumu kujua mipaka ya uhuru huo, na ndio maana inakuwa ngumu kuwashtaki washukiwa,” anaeleza Joseph Wakaba, Mwanasheria kutoka Kenya.
Vijana kuleta mabadiliko?
Maandamano ya vijana ya Juni 2024, yalitikisa mhimili wa nchi, hususani baada ya maeneo muhimu kama vile Mahakama Kuu kuwamiwa na maeneo mengine ya biashara.
Hatua hiyo ilimlazimu Rais Ruto kufanya mabadiliko ya haraka ikiwemo kupunguza bajeti na kubadili baraza lake la mawaziri, pamoja na mkuu wa polisi kujiuzulu.
Vuguvugu hilo la vijana wanaodai maisha bora na uwajibikaji wa serikali, uliunda kundi la Gen Z, ambao walijinasibu kutokuwa na dini, vyama vya siasa wala makabila.
“Nadhani jambo hilo linakuzwa kiasi kwani vijana wale wamesambaratika kwa kiasi kikubwa na baadhi yao wamekuwa sehemu ya wanasiasa wa nchi hii,” Ombongi anasema.



















