Wanajeshi wanne wa Marekani pamoja na wakandarasi watatu walijeruhiwa katika shambulio la kombora la balistiki la Iran dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Kuwait wiki iliyopita. Shambulio hilo lilikusudiwa kujibu shambulio la anga la Marekani kusini mwa Iran, kulingana na ripoti ya vyombo vya habari iliyotolewa Jumapili.
Watu wote saba walipata majeraha madogo na walirejea kazini ndani ya saa 24, kwa mujibu wa kituo cha habari cha CBS News.
Kikosi cha Iran (IRGC) kilisema kililenga kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Kuwait kujibu shambulio la anga la Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Bandar Abbas, kusini mwa Iran.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, IRGC ilisema shambulio hilo la kulipiza kisasi lilifanyika saa 4:50 asubuhi kwa saa za eneo hilo (0120 GMT), saa chache baada ya kile ilichokitaja kuwa shambulio la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa mji wa bandari huo kwa kutumia makombora ya angani.
Hata hivyo, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema kuwa shambulio hilo la kombora “lilizuiwa kwa mafanikio na vikosi vya Kuwait.”
Mvutano wa kikanda uliongezeka mnamo Februari 28 wakati Marekani na Israel zilipoanzisha mashambulizi dhidi ya Iran, hatua iliyosababisha Iran kujibu kwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (droni) na makombora yaliyolenga maeneo mbalimbali katika ukanda huo, pamoja na kufunga Mlango-Bahari wa Hormuz.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yalianza kutekelezwa Aprili 8 kupitia upatanishi wa Pakistan, lakini mazungumzo yaliyofanyika Islamabad hayakufanikiwa kufikia makubaliano ya kudumu.
Baadaye, Rais wa Marekani, Donald Trump, aliongeza muda wa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano bila ya kuyawekea muda huku akiendelea kudumisha zuio dhidi ya meli zinazosafiri kwenda au kutoka bandari za Iran kupitia njia hiyo muhimu ya baharini, na mara kwa mara akisema kuwa makubaliano ya amani yalikuwa karibu kufikiwa.












