Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Kristalina Georgieva, amesema kuwa mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya Saudi Arabia yanaweza kuwa na athari hasi kwa watu duniani kote, huku mzozo katika eneo hilo lenye utajiri wa nishati ukizidisha wasiwasi kuhusu hali ya uchumi wa dunia.
“Uchumi wa Saudi Arabia ni muhimu kwa eneo hili na kwa dunia nzima,” alisema Georgieva katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Bangkok, Thailand, wakati wa Mikutano ya Mwaka ya IMF na Benki ya Dunia.
Tahadhari hiyo imetolewa wakati viongozi, maafisa na wataalamu mbalimbali wakikutana katika mji mkuu wa Thailand kujadili changamoto zinazoikabili dunia kiuchumi. Miongoni mwa masuala yanayojadiliwa ni kupanda kwa gharama ya nishati na wasiwasi kuhusu kasi ya ukuaji wa sekta ya Akili Mnemba (AI).
Kuongezeka kwa mvutano kati ya Saudi Arabia na wapiganani wa Houthi kumezidisha hofu kuhusu athari za mgogoro wa Mashariki ya Kati kwa ukuaji wa uchumi wa dunia.
Wakati huohuo, bei za mafuta ghafi zimepanda kwa kasi tangu Iran ilipofunga Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya kimataifa ya usafirishaji wa mafuta, kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran mwezi Februari.




















