| Swahili
AFRIKA
3 dk kusoma
Waandamanaji nchini Afrika Kusini wanavamia nyumba hadi nyumba kuwasaka wahamiaji
Kutokana na maandamano hayo, polisi wameongeza operesheni za kuwakamata wahamiaji wasiokuwa na nyaraka halali, huku pia wakipeleka maafisa katika maeneo ya maandamano kwa ajili ya kuimarisha usalama.
Waandamanaji nchini Afrika Kusini wanavamia nyumba hadi nyumba kuwasaka wahamiaji
Afrika Kusini, ambayo inakabiliwa na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira, imekuwa ikishuhudia kuongezeka kwa hisia za kupinga wahamiaji. /

Makundi ya waandamanaji wanaopinga uwepo wa wahamiaji nchini Afrika Kusini siku ya Alhamisi waliwatoa raia wa kigeni kutoka majumbani mwao jijini Johannesburg na kuwakabidhi kwa polisi.

Hatua hiyo inaashiria kuongezeka kwa ukali wa maandamano ambayo yamezua hofu katika jamii na kuathiri uhusiano wa Afrika Kusini na baadhi ya mataifa jirani.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, katika eneo la Alexandra jijini Johannesburg, waandamanaji walivunja milango ya nyumba na kuingia katika makazi ambayo walihisi yalikuwa yanawahifadhi wahamiaji wasiokuwa na vibali halali vya kuishi nchini.

Baada ya kuwakamata, waliwasindikiza hadi kwenye magari ya polisi ambako walichukuliwa na kuondolewa eneo hilo. Miongoni mwa waliokamatwa walikuwa mwanamke na mtoto mdogo kutoka Malawi.

Mwanaume mwingine aliyekamatwa na waandamanaji aliiambia Reuters kuwa alikuwa akiishi nchini humo kihalali.

"Mimi ni mmiliki wa kibali cha ZEP," alisema raia wa Zimbabwe, Total Mhlanga, akimaanisha kibali cha Zimbabwean Exemption Permit (ZEP) kinachoruhusu maelfu ya raia wa Zimbabwe kuishi na kufanya kazi nchini Afrika Kusini.

Katika eneo la Soweto, waandamanaji wanaopinga wahamiaji walifanya maandamano wakiwa na fimbo na bendera, wakitangaza mpango wa kuwasaka wahamiaji wasiokuwa na nyaraka halali. Maandamano mengine pia yalifanyika mjini Durban, pwani ya mashariki mwa nchi.

Afrika Kusini, ambayo inakabiliwa na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira, imekuwa ikishuhudia kuongezeka kwa hisia za kupinga wahamiaji katika miezi ya hivi karibuni. Hali hiyo ilifikia kilele kupitia maandamano ya kitaifa yaliyofanyika Juni 30, tarehe ambayo ilikuwa imewekwa kama muda usio rasmi kwa wahamiaji wasiokuwa na vibali kuondoka nchini.

Kiongozi maarufu wa harakati hizo, mtangazaji wa zamani wa redio Jacinta Ngobese-Zuma, alisema siku hiyo kuwa maandamano yataendelea kufanyika kila Alhamisi hadi pale madai yao yatakapotekelezwa.

"Tunapita nyumba kwa nyumba kuwaondoa raia wa kigeni," alisema kiongozi wa jamii, Bongani Msomi, wakati wa maandamano yaliyofanyika Alexandra.

Rais Cyril Ramaphosa ameonya dhidi ya kuwalaumu wahamiaji kwa matatizo ya muda mrefu yanayoikabili nchi hiyo. Serikali yake pia imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa raia hawana mamlaka ya kujichukulia sheria mkononi kwa kutekeleza shughuli za kudhibiti uhamiaji.

Kutokana na maandamano hayo, polisi wameongeza operesheni za kuwakamata wahamiaji wasiokuwa na nyaraka halali, huku pia wakipeleka maafisa katika maeneo ya maandamano kwa ajili ya kuimarisha usalama.

Msemaji wa polisi wa Johannesburg hakupatikana kutoa ufafanuzi kuhusu vitendo vya waandamanaji au hatua zilizochukuliwa na polisi waliokuwa eneo la tukio.

Serikali ya Malawi ilisema siku ya Alhamisi kuwa zaidi ya raia wake 38,000 wamerejea kutoka Afrika Kusini katika wiki za hivi karibuni kupitia zoezi kubwa la kuwarejesha nyumbani kutokana na hofu ya usalama.

Aidha, zaidi ya raia 60,000 wa Zimbabwe pia wamerejea nchini kwao.

CHANZO:Reuters