Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Qalibaf, ameionya Marekani kwamba Mlango-Bahari wa Hormuz utafunguliwa kwa utaratibu utakaowekwa na Iran pekee, na si kwa vitisho vya Marekani.
Qalibaf aliandika kwenye mtandao wa X, alisema: "Marekani bado haijajifunza kuwa uonevu na kuvunja ahadi hautapita tena bila thamani."
Aliongeza: "Naweka wazi: Mkishambulia, nanyi mtashambuliwa."
Qalibaf pia aliionya Marekani dhidi ya kujaribu kuishinikiza Iran kuhusu Mlango-Bahari wa Hormuz.
"Mlango-Bahari wa Hormuz utafunguliwa kwa utaratibu wa Iran pekee, si kwa vitisho vya Marekani," alisema, akiongeza: "Acheni kufanya vitendo visivyo na maana, la sivyo mtajikuta mkizama zaidi kwenye matatizo."
Marekani yalenga maeneo ya kusini mwa Iran
Kauli hizo zimetolewa baada ya vyombo vya habari vya Iran kuripoti kwamba Marekani ilifanya wimbi jipya la mashambulizi usiku wa Jumatano, yakilenga maeneo kadhaa kusini na kusini mashariki mwa Iran.
Baadaye, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilithibitisha kuwa vikosi vya Marekani vilifanya mashambulizi mengine yaliyolenga kupunguza zaidi uwezo wa Iran wa kutishia uhuru wa usafiri wa majini katika Mlango wa Hormuz.
Wakati huo huo, Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu cha Iran kilionya kuwa shambulio lolote jipya kutoka Marekani litakabiliwa na jibu pana zaidi.
Kikosi hicho kilisema kwamba iwapo Marekani itaendeleza mashambulizi yake, hatua za kulipiza kisasi zitaelekezwa pia kwenye kambi nyingine za kijeshi za Marekani katika eneo hilo.












