Shirika la Afya Duniani (WHO) lilifichua Jumatatu kwamba mlipuko wa Ebola unaoenea kwa kasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umesababisha vifo 220, huku maafisa wa afya wakijitahidi kukabiliana na kasi ya kuenea kwa janga hilo.
Wakati mambukizi 101 na vifo 10 vilivyothibitishwa vimerekodiwa, mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema kiwango halisi cha maambukizi ni kikubwa zaidi.
"Sasa kuna zaidi ya watu 900 wanaoshukiwa kuwa na virusi hivyo na vifo vya watu 220 wanaoshukiwa kufariki kwa ugonjwa huo," Tedros alisema katika mkutano wake na mawaziri wa nchi husika.
Mlipuko huo wa Ebola aina ya Bundibugyo, uliotangazwa kama dharura ya afya ya umma ya wasiwasi wa kimataifa Mei 17, pia umeenea hadi Uganda, ambayo ina maambukizi saba yaliyothibitishwa na kifo kimoja.
Tedros anatazamiwa kusafiri hadi DRC pamoja na Mkurugenzi wa dharura wa WHO, huku Shirika hilo likijitolea kukomesha mlipuko huo. "Hali itakuwa mbaya zaidi kabla ya kudhibitiwa," alikiri na kuongeza, "Lakini tunajua virusi hivi, na tunajua jinsi ya kuvizuia."
Changamoto ya kukumbana na mlipuko wa Ebola
Tedros aliangazia changamoto kubwa: kuchelewa kugundua kwa mlipuko huo kunamaanisha kuwa wahudumu wa afya sasa wanapambana na janga linaloenea kwa kasi.
"Tunaongeza operesheni haraka, lakini kwa sasa, janga hilo linatupita," alisema.
Aina ya Ebola inayohusika ni virusi vya Bundibugyo, ambavyo hakuna chanjo iliyoidhinishwa au matibabu.
Milipuko ya awali ya aina hii ilitokea mara mbili tu - nchini Uganda (2007) na DRC (2012).
WHO imependekeza kutanguliza kingamwili mbili za monokloni kwa majaribio ya kimatibabu.
Kuongezeka kwa changamoto ni kuwa majimbo yaliyoathiriwa ya Ituri na Kivu Kaskazini yamekumbwa na ukosefu mkubwa wa usalama na jamii kutoaminiana.
Miezi ya hivi karibuni mapigano makali yameshuhudiwa yaliyowalazimu zaidi ya watu 100,000, kuhama makazi yao pamoja na matukio mawili ya ukosefu wa usalama katika vituo vya afya wiki iliyopita.
WHO imeongeza tathmini yake ya hatari ya kitaifa hadi "juu sana," wakati kiwango cha hatari ya kikanda kikibaki "juu" na cha kimataifa kikiwa "chini."
Nchi jirani zinahimizwa kuchukua hatua mara moja.

















