Wawakilishi wa biashara kutoka Uturuki na Armenia walikusanyika katika mkoa wa mashariki mwa Uturuki wa Kars siku ya Jumanne kwa mazungumzo yanayolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kuunga mkono mchakato unaoendelea wa kurudisha hali kama ilivyokuwa kati ya mataifa hayo mawili.
Mkutano wa “Wafanyabiashara wa Uturuki na Armenia”, unaoratibiwa na Chama cha Wafanyabiashara na Viwanda cha Kars (KATSO), uliwaleta pamoja maafisa, wawakilishi wa chama na wafanyabiashara kutoka nchi zote mbili kujadili biashara, viwanda, usafirishaji, utalii na kuunganisha kanda.
Miongoni mwa waliohudhuria ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Caucasus katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki Ayse Uzer, Mshauri wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Armenia Hayk Darbinyan, Mwenyekiti wa KATSO Kadir Bozan, Mjumbe wa Bodi ya Biashara na Bidhaa wa Uturuki (TOBB) Saim Ozakalın.
Akizungumza katika mkutano huo, Uzer alieleza kuwa kongamano hilo kuwa la “kihistoria” katika uhusiano wa Uturuki na Armenia, akisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa wawakilishi wa biashara kutoka nchi hizo mbili katika ngazi hii.
Alisema mawasiliano ya kidiplomasia kati ya Uturuki na Armenia yameashiria dhamira ya kuimarisha uhusiano na usalama katika kanda.
“Hatua hizi siyo tu zitachangia mafanikio na usalama wa nchi zote mbili, lakini pia kanda nzima ya Caucasus ya Kusini na Ulaya na Asia,” Uzer alisema.
Darbinyan alisema Uturuki na Armenia wana “fursa nyingi” kwa ushirikiano kiviwanda na kibiashara, akieleza uwezo wa biashara ya moja kwa moja kwa njia ya reli kati ya nchi hizo mbili jirani.
Aliongeza kuwa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kutasaidia kupanua ufikiwaji wa biashara hadi Ulaya na kuimarisha ushirikiano zaidi kati ya wafanyabiashara wa nchi hizo mbili.
Bozan alisema washiriki walikusanyika siyo tu kwa jukwaa la kibiashara, lakini pia kujadili mustakabali wa kanda na kuweka misingi ya ushirikiano wa muda mrefu.
“Leo, ushindani duniani siyo tena kati ya nchi na nchi, lakini kati ya kanda. Kwa hiyo, tunatakiwa tusiangaliane wenyewe kwa wenyewe kama wapinzani, lakini kama washirika wa kiuchumi,” alisema.
Mkutano huo unakuja huku kukiwa na juhudi za Uturuki na Armenia kurudisha uhusiano kama ulivyokuwa, ikiwemo majadiliano kuhusu kufungua tena njia za uchukuzi na kurudisha safari za reli.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan pia walijadili uhusiano wa nchi hizi mbili na yanayoendelea katika kanda katika mazungumzo kwa njia ya simu siku ya Jumatatu, kulingana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki.
Wakati wa mazungumzo hayo, Erdogan alisema mchakato wa kurudisha hali kama ilivyokuwa unaendelea kupitia hatua zinazolenga kuwepo kwa biashara ya moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili.
Kufuatia hotuba hizo, mkutano uliendelea kwa mazungumzo ya wawakilishi wa biashara wa Uturuki na Armenia kwa lengo la kushirikiana na fursa za uwekezaji.





















