Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limethibitisha kwa pamoja kumuunga mkono Rais wa FIFA Gianni Infantino siku ya Alhamisi, licha ya kukiri makosa ya namna walivyoshughulikia mpango wa kuuza hisa za mashindano ya FIFA kwa wawekezaji binafsi.
Kamati Kuu ya CAF iliidhinisha taarifa iliotolewa siku ya Jumatano na Infantino pamoja na Katibu Mkuu wa FIFA Mattias Grafstrom kuhusu mapendekezo ya biashara hiyo ya FIFA.
“Tuna nia ya kuendelea kufanya kazi pamoja na FIFA, Mashirikisho na wadau wengine ili kulinda na kuheshimu utaratibu, mchakato muhimu, na uwazi kote duniani na kuendelea kuchangia maendeleo na ukuaji wa Soka kote ulimwenguni,” CAF ilisema katika taarifa.
FIFA ilitoa taarifa baada ya mkutano wa dharura siku ya Jumatano jijini Rabat, Morocco huku kukiwa na shinikizo kwa Infantino kuachia ngazi kufuatia pendekezo, lililohusisha uuzwaji wa hisa za mashindano ya FIFA, ikiwemo Kombe la Dunia.
Katibu Mkuu wa FIFA Grafstrom na wajumbe wa Bodi ya Usimamizi wa FIFA waliohudhuria mkutano huo walithibitisha kumuunga mkono Infantino huku wakikiri makosa katika kushughulikia mapendekezo hayo.














