Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba ameziagiza mamlaka, taasisi na wadau wote waliopewa dhamana ya kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025 wabadilike na wahakikishe wanatekeleza wajibu wao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora na utawala wa sheria.
Kulingana na Nchemba, taarifa za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), zinaonesha kuwa changamoto katika ununuzi wa umma siyo suala la sera, sheria wala kanuni, bali ni wale waliopewa dhamana ya kusimamia sera a kanuni hizo.
Akizundua Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025, Aprili 8, 2026, Nchemba amesema kuwa sehemu kubwa ya shughuli za ununuzi zinaathiriwa zaidi na mitazamo, hulka na tabia za wataalamu na watendaji ikilinganishwa na upungufu wa masuala ya kisera na kisheria.
“Leo tunaweka alama muhimu katika historia ya usimamizi wa mali na rasilimali za taifa letu”, alisema.
Nchemba amebainisha kuwa hatua hiyo ya kisera inalenga kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, kuongeza fursa za ajira na kipato, pamoja na kujenga uchumi jumuishi na shindani unaomilikiwa na Watanzania walio wengi.
“Kwa ujumla, fursa hizi zinalenga kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, kuongeza uzalishaji wa bidhaa, Utoaji wa huduma pamoja na kukuza uwiano wa upatikanaji wa bidhaa na huduma”, alieleza.
Nchemba alisisitiza kuwa, sera hiyo inaweka mkazo katika matumizi ya malighafi na wataalamu wa ndani, kukuza viwanda vya ndani, kuimarisha miundombinu ya kiteknolojia, pamoja na kuzingatia hifadhi ya mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.












