Onyo lilikuwa wazi na lisingeweza kuepukwa.
“Wape salamu kuwa naandaa tukio litakalowashtua kabisa. Operesheni ya kutia hofu. Jambo ambalo halijawahi kutokea.”
Maneno haya, yalimlenga kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar, na yalifikishwa kupitia Mpalestina wiki kadhaa kabla ya Oktoba 7, 2023. Kulingana na uchunguzi wa hivi karibuni wa Haaretz, wangesafiri kupitia Abu Dhabi na kufikia uongozi wa juu wa serikali ya Israel.
Sinwar, ambaye aliuawa na Israel baadaye, inasemekana alitumia neno zilzal, la Kiarabu kumaanisha tetemeko la ardhi, kuelezea kilichokuwa kinakuja.
Wiki kadhaa baadaye, wapiganaji wa Hamas walivuka mipaka ya Gaza na kufanya mashambulizi yaliyowashtua Israel na kuwa na athari kote Mashariki ya Kati.
Kwa yaliyofuata, matukio ya Oktoba 7 yalionekana kama uzembe wa shirika la ujasusi na usalama la Israel.
Lakini miaka mitatu baadaye, kumeibuka taarifa kwenye vyombo vya habari vya Israel ambazo zimeibua maswali: Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alifahamu nini kuhusu mashambulizi hayo?
Taarifa katika vyombo vya Haaretz na Yediot Ahronot vinaonesha Netanyahu na maafisa wake walionywa kuhusu uwezekano wa mashambulizi ya Hamas.
Taarifa hizi ziliibuka mwezi Septemba, wiki kadhaa kabl ya uchaguzi mkuu wa Israel wa Oktoba 27, kufanya Netanyahu kumulikwa kwa namna alivyoshughulikia onyo alilopewa wakati akitafuta kuchaguliwa kwa muhula mwingine.
Taarifa hizi zinaonesha siyo kuonywa mara moja, lakini ujumbe ambao ulipitishwa kwa njia za Wapalestina, uongozi wa UAE na, kulingana na taarifa zingine, shirika la ujasusi la Misri.
Baada ya kushauriana mara kadhaa na washauri wake, kiongozi wa UAE Mohamed bin Zayed Al Nahyan, Mwanamfalme wa Abu Dhabi, akaamua kumfahamisha Netanyahu kuhusu mpango wa Sinwar katikati mwa mwezi Septemba.
Pamoja na Netanyahu kuwa na mkutano kuhusu masuala ya usalama, uliojadili onyo, mwisho uongozi wa Israel haukutoa maamuzi yoyote ya msingi na kuwa na maandalizi ya kukabiliana na mashambulizi ya Hamas.
“Kila mtu duniani waliwapa taarifa (Waisrael),” Dania Koleilat Khatib, mtaalamu wa masuala ya uhusiano wa Waarabu na Marekani aliye na uzoefu zaidi kuhusu uongozi wa eneo la Ghuba, anaiambia TRT World.
Kulingana na Khatib na vyanzo vya Israel, wajumbe wa Palestina wanaojulikana kama “Coal Eyes” ni Sufyan Abu Zaida, Waziri wa zamani wa Masuala ya Wafungwa katika Mamlaka ya Palestina, ambaye mchambuzi amewahi kukutana naye wakati mmoja mjini Prague.
Khatib pia anasema kuwa rafiki wa karibu wa Zaida Abu Dhabi ni Mohammed Dahlan, afisa wa zamani wa Fatah na mshauri wa Mohammed Bin Zayed.
“Hamna cha kuficha tena. Kuna ishara zaidi na zaidi kuwa Netanyahu alifahamu kuhusu hilo. Misri ilimwambia, Coal Eyes (Zaida) alimwambia, na uongozi wa Imarati ulimfahamisha,” anasema Khatib.
Wote Haaretz na WSJ waliripoti kuwa mapema mwezi Oktoba 2023 mkuu wa ujasusi wa Misri Abbas Kamel binafsi alimuonya Netanyahu kuhusu mashambulizi ya Hamasa lakini hakuzingatia.
Netanyahu anakanusha taarifa za kuonywa na Misri na UAE, akidai kuwa uongozi wa UAE na ujasusi wa Misri haukumpa taarifa. Aliitaja taarifa ya onyo la UAE kuwa “uongo mtupu” na kusema kuwa “hakuna chanzo cha ujasusi cha Israeli kilichompa Waziri Mkuu onyo kutoka Misri”.
Ramzy Baroud, mchambuzi wa siasa kutoka Palestina na mwandishi, anaeleza kuwa kuangazia tu kwa onyo kupitia serikali za kikanda kunaweza kufumbia macho suala la taarifa hiyo.
“Kwa vyombo vya habari kuangazia onyo la mataifa mengine katika kanda kunazuia kutathmini hali halisi —Wapalestina wenyewe walitoa onyo la wazi, moja kwa moja,” Baroud ameiambia TRT World.
Onyo la "tetemeko la ardhi" la Sinwar na ‘‘mafuriko" “lilikuwa wazi na lilifahamika,” aliongeza.
Kwa Baroud, kutozingatia onyo hili kunaonesha mienendo ya kutoamini kuwa shirika la Palestina linaweza kutoa muelekeo.
Licha ya miongo kadhaa ya sera za juhudi za Israel tangu kuundwa kwa taifa hilo 1948, Israel imeshindwa kuungwa mkono kikamilifu na wengi wa Wayahudi katika taifa la kihsitoria la Palestina, anasema Sami al Arian, Profesa wa Palestina na mkurugenzi wa Kituo cha Kiislamu na Masuala ya Dunia katika Chuo Kikuu cha Sabahattin Zaim jijini Istanbul..
Wakati huohuo,Sami al Arian, anaeleza namna Netanyahu alivyoshughulikia onyo, akizungumzia kile alichokieleza kuwa kiburi cha waziri mkuu na kuwa na imani na mipango yake ya kisiasa.
Kulingana na Arian, Netanyahu alikuwa anaamini zaidi kuhusu “itikadi yake”, na kudharau onyo lolote ambalo lilipingana na mtazamo wake.
“Anajiona yeye ndiyo kila kitu yeye ndiye mwenye busara zaidi duniani. Tahadhari yoyote ambayo ilionekana kwenda kinyume na mkakati wake na anavyofikiria yeye hakutilia maanani hilo.”
Onyo kuhusu mashambulizi ya Hamas lilikuwa kama “kelele” kwa Netanyahu, Arian anasema, kwa sababu aliamini kuwa Israel ingeweza kusawazisha hali na Saudi Arabia na mataifa mengine katika kanda huku ikiendeleza ushawishi wake kote Mashariki ya Kati, licha ya Palestina kuendelea kutetea haki zake.
“Na Oktoba 7 ikafika na kila kitu kikatibuka.”



















