| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Uganda yamuomboleza Moses Ali 'Simba wa Adjumani'
Amekuwa akipendwa na wafuasi wake ambao wamekuwa wakimuita "Simba wa Adjumani.”
Uganda yamuomboleza Moses Ali 'Simba wa Adjumani'
Amekuwa akipendwa na wafuasi wake ambao walizoea kumuita "Simba wa Adjumani.”

Chama tawala cha Uganda NRM pamoja na raia wa nchi hiyo wanaomboleza kifo cha mwanasiasa mkongwe Jenerali Mstaafu Moses Ali. Taarifa za mbunge wa muda mrefu wa Adjumani Magharibi zilienea mitandaoni Julai 18, 2026, huku salamu za rambi rambi zikiendelea kutumwa na watu wa matabaka mbalimbali, ikiwemo wanasiasa, viongozi wa dini na mashirika, pamoja na taasisi za elimu nchini humo.

Ni dhahiri kwamba, licha ya umri wake, Moses Ali ameendelea kuwa na ushawishi wa kisiasa.

Utumishi

Kwa zaidi ya miongo mitano, Jenerali mstaafu Moses Ali ameshika nafasi mbali mbali katika utumishi wa umma nchini Uganda.

Aliwahi kuwa mwanajeshi, mwanasheria, waziri na mbunge.

Amekuwa akipendwa na wafuasi wake ambao walizoea kumuita "Simba wa Adjumani.”

Wapinzani wanamkosoa kwa nafasi yake katika uongozi wa Idi Amin.

Safari ya kisiasa

Safari yake ya kisiasa imekuwa na misukosuko kuanzia vurugu za baada ya uhuru wa Uganda na hatimae kuingia katika uongozi wa Rais Yoweri Museveni.

Safari yake ya utumishi wa umma imegusa takriban vipindi vyote vya uongozi tangu uhuru.

Ametumikia jeshi la nchi hiyo chini ya Rais Milton Obote, akapanda ngazi baada ya mapinduzi ya Idi Amin mwaka 1971, akaenda uhamishoni baada ya kuondolewa kwa Amin, akarudi kama kiongozi wa waasi dhidi ya serikali ya Obote, kipindi cha pili.

Kuingia chama tawala cha NRM

Baadae kupatana na Rais Museveni baada ya NRM kuchukua madaraka mwaka 1986, na baadae kuwa miongoni mwa watu waliotumikia nafasi ya uwaziri na naibu waziri mkuu kwa muda mrefu.

Akiwa na umri wa miaka 87, Ali aliendelea kuwa mbunge wa Adjumani Magharibi baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu wa Januari 15, 2026. Hata hivyo, mara hii hakuteuliwa katika bazara za mawaziri.

Ushawishi wa kisiasa

Wafuasi wake, walimuona kama kiongozi mwenye ukakamavu, uzalendo, na uzoefu wa hali ya juu. Hata hivyo, baadhi walimuona kama mwanasiasa asiyefaa tena kuwepo katika uongozi kutokana na umri wake na afya yake.

Licha ya ukosoaji huo, kwa Moses Ali na wafuasi wake, ilikuwa ni kama kelele za chura ambazo hazimzuii tembo kunywa maji.