Rais wa China, Xi Jinping, Rais wa Marekani, Donald Trump, na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, wamehitimisha mkutano wao wa kwanza wa ana kwa ana wa viongozi wa nchi hizo tatu, uliofanyika mjini Shenzhen, China.
Viongozi hao watatu walitoa matamshi yao katika kikao na waandishi wa habari kilichodumu kwa takribani dakika 15, siku ya Alhamisi, kabla ya kuendelea na mazungumzo ya faragha.
Xi alieleza kuwa ushirikiano chanya kati ya mataifa hayo matatu yenye nguvu kubwa duniani si jambo la hiari, bali ni jambo la lazima. Alisema mataifa makubwa yana wajibu maalumu katika kukabiliana na changamoto za dunia na kudumisha amani ya kimataifa.
“Sisi ni jumuiya yenye mustakabali wa pamoja. Katika dunia hii, mataifa makubwa yana wajibu wa kubeba majukumu maalumu,” alisema Xi.
Kwa upande wake, Putin alisema Urusi, China na Marekani zinaweza kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha utulivu duniani kupitia ushirikiano unaozingatia kuheshimiana, usawa na maslahi yenye uwiano.
Trump alisema nchi hizo tatu ziko katika nafasi ya kipekee ya kujadili namna ya kupunguza akiba ya silaha za nyuklia na kupunguza hatari ya silaha hizo kutumiwa.
Upokonyaji wa silaha za nyuklia na kuzuia kuenea kwake
Trump alitoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya mataifa matatu yenye akiba kubwa zaidi ya silaha za nyuklia duniani. Alisema nchi hizo zina wajibu wa kupunguza idadi ya silaha hizo na kuzuia matumizi yake.
“Marekani, Urusi na China, ambazo kwa kiasi kikubwa ndizo nchi tatu zenye silaha nyingi zaidi za nyuklia duniani, ziko katika nafasi ya kipekee ya kujadili namna ya kupunguza kiwango cha silaha hizo duniani na pia kupunguza hatari ya kutumiwa kwake,” alisema Trump.
Alikiri kuwa kuachana na akiba kubwa ya silaha za nyuklia si jambo rahisi, akisema ni vigumu kwa viongozi wa mataifa kuamua kusalimisha maelfu ya silaha hizo.
Rais huyo wa Marekani alieleza kuwa ushirikiano wa pande tatu ni “muhimu sana” katika kukabiliana na kuenea kwa silaha za nyuklia. Aidha, alisema Marekani haitaruhusu Iran kumiliki silaha ya nyuklia.
“Hatutairuhusu Iran kuwa na silaha ya nyuklia,” alisema.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI), kufikia Januari 2026, China ilikuwa na takriban vichwa vya nyuklia 620, ikilinganishwa na 5,042 vya Marekani na 5,420 vya Urusi.
China imekuwa ikikataa mara kwa mara wito wa kujiunga na mazungumzo ya upokonyaji wa silaha za nyuklia, ikieleza kuwa akiba yake ya silaha hizo ni ndogo kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na zile za Marekani na Urusi.
Vita vya Urusi na Ukraine na migogoro ya kikanda
Putin alisema nchi hizo tatu zina maslahi ya pamoja katika kutafuta suluhisho la migogoro ya kikanda, ukiwemo vita kati ya Urusi na Ukraine. Alibainisha kuwa suala hilo lilijadiliwa pia katika mazungumzo yake ya pande mbili na Xi pamoja na Trump.
Trump alisema mkutano wake wa awali wa pande mbili na Putin ulijikita kwa kiasi kikubwa katika mgogoro huo. Alieleza matumaini yake kuwa Urusi na Ukraine zinataka kuona vita hivyo vikifikia mwisho.
“Kwa kiasi kikubwa, hilo ndilo lilikuwa lengo la mazungumzo yetu, na ninaamini kuna hatua zinazopigwa,” alisema Trump.
Putin pia alisema mataifa hayo matatu yanapaswa kujadili masuala ya uhusiano wa kiuchumi duniani na kikanda, usalama wa chakula pamoja na usalama wa nishati.
Alisisitiza kuwa nchi hizo zina wajibu wa pamoja katika kudumisha amani ya kimataifa, akibainisha kuwa Urusi, China na Marekani zilikuwa miongoni mwa mataifa yaliyoshinda Vita vya Pili vya Dunia.
Sheria za kimataifa na taasisi za kimataifa
Putin alisema nchi hizo tatu zina wajibu wa kulinda mfumo wa sheria za kimataifa ulioanzishwa sanjari na Umoja wa Mataifa (UN).
“Sisi tulikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Umoja wa Mataifa. Kwa hiyo, ni wajibu wetu kuhifadhi na kuimarisha mfumo wa sheria za kimataifa ulioanzishwa sanjari na taasisi hii ya kimataifa,” alisema.
Wakati huohuo, Trump alitangaza mpango wa kupendekeza hatua za pamoja na China na Urusi kwa ajili ya kulinda mamlaka na uhuru wa nchi zao dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Hata hivyo, nchi hizo zote tatu si wanachama wa mahakama hiyo.
Trump aliielezea mahakama hiyo yenye makao yake makuu mjini The Hague, Uholanzi, kuwa imevuka mipaka ya mamlaka yake na kufanya mambo yasiyokuwa ndani ya wigo wake wa kisheria.
Marekani imeiwekea ICC vikwazo, ikiwa ni sehemu ya msimamo wake wa muda mrefu wa kupinga mamlaka ya mahakama hiyo katika kushughulikia kesi zinazowahusu raia wa Marekani.
Msimamo huo wa Marekani ulizidi kuwa mkali baada ya ICC kutoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo, Yoav Gallant, mwezi Novemba 2024. Hati hizo zilihusiana na tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu katika Ukanda wa Gaza.
Wito wa mazungumzo kati ya mataifa makubwa
Xi alizitaka nchi hizo tatu kuwa mfano wa kuigwa kwa kushirikiana katika kukabiliana na changamoto za kimataifa na kudumisha amani pamoja na utulivu duniani.
Alisema China inalenga kujenga uhusiano wa kimkakati na Marekani wenye misingi ya ushirikiano na utulivu wa muda mrefu, huku ikiendelea kuimarisha ushirikiano wake wa kimkakati wa kina na Urusi.
Trump pia alisisitiza umuhimu wa kuendeleza mazungumzo kati ya mataifa hayo, akisema mawasiliano ni muhimu katika kutafuta suluhisho la migogoro ya kimataifa.
“Hakuna tatizo lililowahi kutatuliwa kwa mtazamo wa kizamani wa kukataa kulizungumzia tatizo. ... Hakuna amani iliyowahi kupatikana kwa kutochukus fursa za kushirikiana na kufanya mazungumzo,” alisema Trump.



















