Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema Jumatatu kuwa usambazaji wa gesi kwenda Syria ulioanzishwa kupitia mpango wa Uturuki na Azerbaijan utasaidia maendeleo ya nchi na usalama katika kanda.
“Mchango wa usambazaji wa gesi nchini Syria, ambao ulianza mwezi Agosti kutokana na mpango wa Uturuki na Azerbaijan, kwa maendeleo ya nchi hizi na usalama katika kanda haupingiki,” Erdogan amesema kupitia ujumbe katika ufunguzi wa Wiki ya Nishati ya Baku.
Erdogan anasema yaliyojiri hivi karibuni kwa mara nyingine yameonesha umuhimu wa hatua zilizochukuliwa pamoja na Azerbaijan katika masuala ya nishati, na nchi hizo mbili zimekuwa na miradi mikubwa ambayo awali yalionekana kama hayawezekani.
Alieleza kuhusu miradi ya gesi asilia ya Baku-Tbilisi-Ceyhan, Baku-Tbilisi-Erzurum na Trans-Anatolia, ambayo ilianzishwa na Azerbaijan na kukamilishwa kwa mchango wa Georgia.
Uhusiano kati ya Uturuki na Azerbaijan umeimarika zaidi kupitia ushirikiano wa Azeri-Chirag-Gunashli na Shah Deniz, ilihali ushirikiano mpya wa Shafag-Asiman unaonesha ushirikiano wa nishati wa mataifa mawili unaendelea bila kusita, aliongeza.
Erdogan anasema bomba la gesi la Igdir-Nakhchivan, ambalo lilianza kutumika mwaka uliopita, limeimarisha upatikanaji wa bidhaa hiyo katika eneo la Nakhchivan nchini Azerbaijan.
Kuunganisha umeme kati ya Uturuki na Azerbaijan bado ni muhimu kimkakati, alisema, akiongeza kuwa Mradi wa Usambazaji Umeme na ule wa Biashara kati ya Uturuki, Azerbaijan, Georgia na Bulgaria unatarajiwa kuchangia katika upatikanaji wa nishati kwenye kanda nzima.
Kuhusu usambazaji wa nishati katika kanda, Erdogan anasema kuwa kuna fursa za kuimarisha ushirikiano kwa kuuza gesi kutoka mataifa yanayozungumza Kituruki kupitia Azerbaijan na Uturuki.
Aliongeza kuwa bomba la Baku-Tbilisi-Ceyhan linatumiwa zaidi kusafirisha raslimali asilia za Kazakhstan hadi katika soko la mataifa ya Magharibi.
Uturuki ina dira ya kuhakikisha uthabiti kote katika masuala ya nishati, ikiwemo nishati endelevu na safi, kulingana na uhakika na kuzingatia mazingira, Erdogan anasema.
Uturuki, aliongeza, itaimarisha dhamira yake ya kuwa miongoni mwa nchi za kupigiwa mfano kwa kuwa wenyeji wa kongamano la COP31 jijini Antalya Novemba 9-20.



























