Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amesema kuwa vurugu zilizojitokeza nchini humo wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, zilimbebesha mzigo mkubwa mabegani mwake.
Akizungumza mara baada ya kupokea ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani kutoka kwa Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, Aprili 23, 2026 jijini Dar es Salaam, kiongozi huyo amebainisha kuwa matukio hayo yalimfanya ahisi kutwishwa mzigo mzito mabegani mwake, akisema anaomba Mungu yasijirudie tena.
“Jambo hili limenitwisha mzigo mzito mabegani mwangu. Lakini nataka niwahakikishie kuwa, nitaubeba kwa ujasiri, kujiamini na tahadhari kubwa kadri Mungu atakavyoniongoza…tuseme never again, yasijirudie,” alieleza.
Kulingana na kiongozi huyo, hakutarajia kutokea kwa kadhia hiyo nchini katika kipindi chake cha uongozi, akieleza kuwa hali hiyo imembebesha mzigo mkubwa wa uwajibikaji.


















