Mahakama moja nchini Ujerumani imewahukumu raia 12 wa Nigeria kwa kosa la kuendesha mtandao wa utapeli wa kimapenzi na utakatishaji fedha.
Kulingana na mahakama hiyo ya jijini Munich, waliohukumiwa wanakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 34 hadi 55, na watatupwa jela kutumikia vifungo vya kuanzia miaka mitatu hadi minane na nusu.
Raia hao wa Nigeria wanadaiwa kupatikana na hatia ya kuendesha mtandao huo wa kimataifa wenye kuwalaghai watu kimapenzi na baadaye kuwatapeli fedha zao.
Watuhumiwa hao, wanadaiwa kutumia utambulisho wa bandia kama vile kujifanya kama wanajeshi wa Marekani waliopo katika operesheni maalumu Mashariki ya Kati, kuwalaghai watumiaji wa mitandao ya kijamii na kisha kuonesha kuwa wangependa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wao.
Waathirika wa mtandao huo, wanadaiwa kuombwa kuhamisha kiasi kikubwa cha fedha kwa ‘wapenzi’ wao kwa kisingizio kuwa walikuwa wana dharura za kiafya na walihitaji nauli kwa ajili ya kusafiri.
Kulingana na mahakama hiyo, wengi wa waathirika wa mtandao huo walikuwa ni wanawake, wazee na watu wenye changamoto ya ulemavu.













