Kiongozi wa Mali, Assimi Goita, atachukua majukumu ya waziri wa ulinzi, kulingana na maelekezo yaliyosomwa kwenye televisheni ya taifa siku ya Jumatatu, baada ya kifo cha aliyekuwa waziri kutokana na mashambulizi.
Hivi karibuni Mali ilitikiswa kiusalama baada ya ngome zake muhimu za kijeshi kushambuliwa na Tuareg wanaotaka kujitenga na magaidi wenye uhusiano na kundi la Al Qaeda, wakati ambao Waziri wa Ulinzi Sadio Camara aliuawa akiwa nyumbani kwake kutokana na gari lililokuwa na mabomu.
Mashambulizi hayo ni makubwa zaidi kuwahi kufanyika katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi katika kipindi cha karibu miaka 15.
Mashambulizi hayo katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Bamako, yalisababisha vifo vya watu wasiopungua 23.
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya watoto, UNICEF lilisema siku ya Ijumaa kuwa raia pamoja na watoto walikuwa miongoni mwa waliouawa na kujeruhiwa.















