Addisu Gobena wa Ethiopia ameshinda mbio za Sydney Marathon kwa wanaume kwa muda wa saa 2:04:42, muda ambao ni rekodi mpya ya njia hiyo, akiboresha sana matokeo yake ya kushika nafasi ya pili katika mbio za mwaka jana.
Gobena alionyesha kiwango cha juu na kumaliza mbio hizo akiwa mbele kwa sekunde nne pekee dhidi ya M-Ethiopia mwenzake, Chimdessa Debele Gudeta, aliyemaliza kwa muda wa saa 2:04:46.
Tebello Ramakongoana wa Lesotho alishika nafasi ya tatu kwa muda wa saa 2:04:57 na kuleta matokeo ya kushtukiza, huku wanariadha wote watatu wakimaliza mbio hizo kwa muda bora zaidi kuliko rekodi ya awali ya njia hiyo.
Muda wa ushindi wa Gobena ulifuta rekodi ya awali ya Sydney ya saa 2:06:06, iliyowekwa na mwanariadha Muethiopia mwenzake Hailemaryam Kiros mwaka 2025, na kumfanya kuwa mwanariadha wa kiume wa mbio ndefu (marathon) mwenye kasi zaidi kuwahi kurekodiwa nchini Australia.
Simbu apokonywa nyama mdomoni
Matokeo haya yanaashiria maendeleo makubwa kwa Gobena, ambaye alirejea Sydney baada ya kushika nafasi ya pili mwaka jana. Sasa anaondoka katika jiji hilo la Australia akiwa na zawadi kubwa zaidi katika taaluma yake, ushindi katika mojawapo ya mbio kuu za dunia (World Marathon Majors) na rekodi mpya ya njia hiyo.
Alphonse Simbu wa Tanzania alirekodi muda sawa na Ramakongoana, akimaliza wa nne baada ya wawili hao kutenganishwa kwenye mstari wa kumalizia.
Muda wa saa 2:04:57 ulikuwa kiwango kizuri kwa Simbu katika ushiriki wake wa kwanza kwenye Sydney Marathon, akishindana na kundi la wanariadha waliokuwa na rekodi binafsi za muda wa chini ya saa 2:05.
Mwanariadha huyo wa Tanzania aliingia kwenye mbio hizo akiwa bingwa mtetezi wa dunia baada ya kuweka historia kwa kushinda mbio za marathon katika Mashindano ya Dunia ya Riadha ya mwaka 2025 jijini Tokyo.
Afrika Mashariki ilitawala mbio hizo za wanaume kwa kuchukua nafasi 16 kati ya 20 za juu. Ethiopia ilikuwa na wanariadha 10, Kenya ilikuwa na wanariadha 5, huku Tanzania ikiwakilishwa na mwanariadha mmoja. Hakukuwa na mshiriki kutoka Uganda.


















