Mfanyabiashara wa Pakistan amehukumiwa kifungo cha zaidi ya miaka 27 jela nchini Marekani kwa kupanga njama ya kumuua mwanasiasa mashuhuri wa Marekani, katika mpango ambao alidai ulielekezwa na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC), kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani.
Asif Merchant, mwenye umri wa miaka 48, alikutwa na hatia mapema mwaka huu kwa makosa ya kupanga mauaji na kujaribu kutekeleza tendo la ugaidi, mwaka 2024. Ushahidi uliotolewa mahakamani ulionyesha kuwa watu walioweza kulengwa ni pamoja na Rais wa Marekani Donald Trump, rais wa zamani Joe Biden na Nikki Haley, aliyewahi kuwa balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa.
Waendesha mashtaka walisema Merchant alijaribu kuwashawishi watu nchini Marekani washiriki katika mpango wa kumuua Trump na viongozi wengine, kama hatua ya kulipiza kisasi kufuatia mauaji ya kamanda wa kijeshi wa Iran, Qassem Soleimani, yaliyotekelezwa na Marekani mwaka 2020.
Jaji wa Mahakama ya Wilaya ya Marekani, Eric Komitee, alisema kuwa kupanga mauaji ya rais au kiongozi wa ngazi ya juu serikalini ni kosa kubwa sana lenye uzito wa kipekee.
Katika ushahidi wake mahakamani, Merchant alisema kuwa mtu aliyekuwa na uhusiano na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu cha Iran (IRGC) alimpa maelekezo ya kupanga mauaji hayo. Alidai kuwa alitekeleza maagizo hayo kwa hofu ya usalama wa ndugu zake waliokuwa nchini Iran.
Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, Merchant aliwalipa Dola 5,000 kwa watu aliokuwa akiamini ni wauaji wa kukodiwa, bila kujua kuwa walikuwa maafisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) waliokuwa wakifanya operesheni ya siri.
Alikamatwa katika jimbo la Texas mwezi Julai 2024, alipokuwa akijiandaa kurejea nchini Pakistan.
Hata hivyo, Iran imekanusha madai kwamba ilipanga njama ya kuwaua viongozi wa Marekani.
Wakili wa Merchant amesema kuwa anapanga kukata rufaa kupinga hukumu hiyo, huku upande wa mashtaka umeomba apewe adhabu ya kifungo cha maisha jela.



















