Ubalozi wa Marekani nchini Saudi Arabia umewaagiza wafanyakazi wake wote pamoja na familia zao kuondoka nchini humo, vyanzo vya kidiplomasia vimeiambia shirika la habari la AFP.
Haya yanajiri wakati Saudi Arabia ikiendelea kukabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa wapiganaji wa Houthi wa nchini Yemen.
“Wafanyakazi wote wa Marekani na familia zao wameagizwa kuondoka katika Ubalozi wa Marekani nchini Saudi Arabia,” chanzo hicho kilisema.
Vyanzo hivyo viliongeza kuwa familia za wafanyakazi wa ubalozi pia zimeagizwa kuondoka katika nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Jordan, Qatar na Bahrain.
Shirika la habari la Reuters, likinukuu maafisa watatu wa Marekani siku ya Jumatano, iliripoti kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inajiandaa kutoa agizo la kuondoka kwa baadhi ya wafanyakazi na wanafamilia wao kutoka katika balozi za Marekani katika eneo lote la Ghuba.
Maafisa wawili wa Marekani walisema hatua hiyo inachukuliwa kutokana na uwezekano wa kurejea kwa mapigano, hasa dhidi ya wapiganaji wa kundi la Houthi nchini Yemen.
Ubalozi wa Marekani jijini Riyadh ulitoa tahadhari ya kiusalama kuhusu uwezekano wa mashambulizi zaidi ya Wahouthi dhidi ya Saudi Arabia, kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni yaliyosababisha vifo, yakiwemo yale yaliyolenga eneo la uwanja wa ndege wa Riyadh.
Maafisa wawili wa Marekani walisema maagizo hayo ya kuondoka yanaweza kuhusisha kuwaondoa wafanyakazi wote pamoja na familia zao katika ubalozi wa Marekani nchini Saudi Arabia.
Siku ya Jumatano, watu wawili waliuawa katika shambulizi lililolenga kituo cha mafuta cha Shaybah nchini Saudi Arabia. Shirika la habari la serikali liliripoti, likimnukuu afisa wa Wizara ya Nishati, kuwa mifumo ya ulinzi wa anga ilifanikiwa kuizuia ndege isiyo na rubani iliyokuwa ikijaribu kushambulia kituo kilichoko mashariki mwa nchi hiyo.
Shambulizi hilo la ndege isiyo na rubani halikuathiri shughuli za uzalishaji katika eneo hilo la mafuta.
Mapigano nchini Yemen
Mapigano kati ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, unaounga mkono serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa, na wapiganaji wa kundi la Houthi, wanaodhibiti mji mkuu Sanaa na sehemu kubwa ya maeneo ya kaskazini, yameongezeka katika wiki za hivi karibuni. Hali hiyo imefungua uwanja mwingine wa mapigano katika vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Katika wiki za hivi karibuni, mashambulizi ya Wahouthi dhidi ya Saudi Arabia yamefikia kiwango kisicho cha kawaida, hali iliyolazimu Riyadh kufunga uwanja wake mkuu wa ndege na kuahirisha mkutano mkubwa wa uwekezaji.
Vilevile, kizuizi cha Wahouthi dhidi ya usafiri wa baharini kinatishia usafirishaji wa mafuta kutoka Saudi Arabia, ambayo ndiyo nchi inayoongoza duniani kwa kuuza mafuta ghafi.
Serikali ya Yemen ilianzisha mashambulizi ya kijeshi mapema mwezi huu kwa lengo la kuteka maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi, ikiwemo mji mkuu Sanaa, kwa msaada wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia.
Yemen imekuwa katika hali ya mzozo tangu mwaka 2014, wakati Wahouthi walipouteka mji mkuu Sanaa pamoja na majimbo mengine kadhaa. Hatua hiyo ilisababisha muungano unaoongozwa na Saudi Arabia kuingilia kati mwezi Machi 2015, ukiunga mkono serikali inayotambuliwa kimataifa.
Wahouthi wanadhibiti sehemu kubwa ya maeneo ya kaskazini na magharibi mwa Yemen, huku vikosi vya serikali na washirika wao vikidhibiti mji wa Aden pamoja na sehemu kubwa ya majimbo ya kusini na mashariki mwa nchi hiyo.























