Eusebia Munuo, mwanamke wa kwanza Mtanzania aliyeweka historia katika mfumo wa sheria
Historia ya Eusebia Munuo inaendelea kuwa kumbukumbu ya safari iliyofungua milango kwa wanawake katika taaluma ya sheria nchini Tanzania. / TRT Afrika Swahili
Eusebia Munuo, mwanamke wa kwanza Mtanzania aliyeweka historia katika mfumo wa sheria
Huyu ni Eusebia Munuo, mwanamke wa kwanza kuwa hakimu nchini Tanzania na baadaye Jaji wa kwanza mwanamke wa Mahakama ya Rufani Tanzania.

Mwaka 1946, katika Kijiji cha Njari mkoani Kilimanjaro, alizaliwa mtoto wa kike ambaye miaka kadhaa baadaye angeandika historia katika sekta ya sheria nchini Tanzania.

Huyu ni Eusebia Munuo, mwanamke wa kwanza kuwa hakimu nchini Tanzania na baadaye Jaji wa kwanza mwanamke wa Mahakama ya Rufani Tanzania.

Safari yake ya kitaaluma, changamoto alizokabiliana nazo na mchango wake katika kuimarisha haki na usawa sasa vimehifadhiwa katika kitabu kinachoitwa “Justice Eusebia Munuo: A Trailblazer in the Legal Profession in Tanzania,” kilichozinduliwa jijini Dodoma na Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju.

Katika uzinduzi huo, Masaju amesisitiza umuhimu wa Mahakama kuendelea kuhifadhi historia za majaji, mahakimu na watumishi waliochangia katika maendeleo ya taasisi hiyo, akieleza kuwa historia ya Mahakama haijengwi kwa hukumu pekee, bali pia kwa kutambua maisha, maamuzi na mchango wa watu walioijenga.

Kitabu hicho kinaelezea safari ya Munuo katika taaluma ya sheria, ikiwemo mchango wake katika kupinga ubaguzi dhidi ya wanawake katika haki ya kurithi mali kwa misingi ya sheria za kimila na kulinda haki za watoto.

Mbali na kuwa miongoni mwa waanzilishi wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), Munuo aliweka historia nyingine mwaka 2012 hadi 2014 alipokuwa Mtanzania wa kwanza kuchaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Kimataifa cha Majaji Wanawake (IAWJ).

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Dkt Paul Kihwelo, amesema kitabu hicho ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo kuhifadhi historia za viongozi waliochangia maendeleo ya Mahakama na sekta ya haki nchini.

Kwa upande wake, Profesa Ruth Meena anaeleza umuhimu wa kutambua mchango wa wanawake waliofungua njia katika nafasi za uongozi na kuleta mabadiliko katika jamii.

Kitabu hicho ni cha pili kuandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto katika juhudi za kuhifadhi historia ya viongozi wa Mahakama nchini, baada ya kile kilichoelezea maisha ya Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, marehemu Robert Habesh Kisanga, kilichozinduliwa Januari 2024.

Kupitia kitabu hicho, historia ya Eusebia Munuo inaendelea kuwa kumbukumbu ya safari iliyofungua milango kwa wanawake katika taaluma ya sheria nchini Tanzania.