Serikali ya Tanzania iko katika hatua za mwisho za mazungumzo na Benki ya Exim ya Uturuki ili kupata ufadhili wa dola za Marekani milioni 280 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kipande cha tatu na cha nne cha mradi wa reli ya kisasa (SGR).
Mazungumzo hayo yamefanyika Jijini Antalya nchini Uturuki, pembezoni mwa Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi COP31, kati ya ujumbe wa Tanzania ukiogozwa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar na Ujumbe wa Benki ya Exim ya Uturuki ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Ali Guney.
Mbali na mradi wa SGR, benki hiyo pia inaangalia kufadhili miradi mingine ya miundombinu nchini Tanzania kama barabara na madaraja ili kukuza biashara kati ya mataifa hayo mawili kufikia angalau dola bilioni moja.
Kulingana na Omar, ujenzi wa mradi huo wa kimkakati wa SGR kipande cha tatu na nne wenye urefu wa zaidi ya kilometa 700, una thamani ya dola za Marekani bilioni 1.6 ambapo kiasi cha dola bilioni 1.32 kimeshapatikana, na kiasi cha dola milioni 280 ndicho kinachosubiriwa ili kukamilisha bajeti hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Uturuki, Ali Guney, amesema kuwa Benki yake inathamini ujenzi wa mradi huo kwa maendeleo ya Tanzania na nchi jirani na kwamba Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo itakutana mwezi huu kujadili maombi ya ufadhili huo unaohitajika ili kukamilisha ujenzi wa Reli hiyo ya kisasa.




















