Mkenya Peres Jepchirchir ameshinda mbio za wanawake katika Marathon ya Sydney, na kuongeza taji jingine muhimu kwenye taaluma yake ya kuvutia.
Bingwa huyo wa dunia alitawala mbio hizo, akivuka mstari wa kumalizia kwa muda wa saa 2:18:31 — zaidi ya dakika tatu mbele ya mwenzake Irine Cheptai, aliyemaliza wa pili kwa muda wa saa 2:22:11.
Shure Demise wa Ethiopia alishika nafasi ya tatu kwa muda wa saa 2:22:33.
Jepchirchir, bingwa wa marathon wa Olimpiki wa mwaka 2021, anaongeza ushindi wa Sydney kwenye orodha ya ushindi wake wa awali katika mbio kuu za dunia za marathon jijini New York, Boston na London.
Muda wake wa ushindi ulikuwa sekunde tisa tu nyuma ya rekodi ya Sydney ya saa 2:18:22, iliyowekwa na Sifan Hassan mwaka jana.
Angalau wanariadha 8 kutoka Afrika Mashariki walishiriki katika mbio za leo na kumaliza katika nafasi 20 za juu, wakiwemo Wakenya 3, Waethiopia 4 na Mganda mmoja na Mtanzania mmoja.
Magdalena Shauri, mshiriki pekee kutoka Tanzania, alikuwa miongoni mwa kundi la wanariadha wa daraja la juu lakini hakufanikiwa kuingia kwenye orodha ya washindi wa juu.
Ushindi huu unasisitiza zaidi hadhi ya Peres miongoni mwa wanariadha mahiri wa marathon wa kizazi chake, huku Sydney ikiandaa toleo lake la pili kama mbio kuu ya dunia ya marathon (World Marathon Major).


















