Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, amesema amekuwa akikabiliwa na vitisho kutokana na msimamo wake wa kupinga utawala wa Kenya Kwanza.
Akizungumza katika mahojiano na Radio Citizen, Sifuna alisema vitisho hivyo vilianza baada ya kuweka wazi msimamo wake dhidi ya serikali. Alidai kuwa baadhi ya watu, ambao hakuwataja majina, wamekuwa wakijaribu kumshinikiza kwa kumtishia maisha.
Kwa mujibu wa seneta huyo, amekuwa akionywa mara kwa mara kwamba anaweza kuuawa kwa kupangiwa ajali ya barabarani au kupigwa risasi. Aidha, alisema amekuwa akipewa tahadhari dhidi ya kula au kunywa katika baadhi ya maeneo kwa madai kuwa maisha yake yanaweza kuwa hatarini.
"Nimekuwa nikitishwa mara kwa mara. Nimeambiwa nitakufa katika ajali ya barabarani, nitapigwa risasi na kuuawa. Pia nimeonywa nisile mahali fulani wala kunywa mahali pengine kwa sababu kulikuwa na nia ya kunidhuru," alisema Sifuna.
Sifuna alisisitiza kuwa hajamkosea mtu yeyote, akisema kinachoonekana kumweka katika hali hiyo ni kuwa na mtazamo tofauti kuhusu namna nchi inavyopaswa kuongozwa.
Alisema, "Sijamkosea mtu yeyote. Ni kwamba tu nina maoni tofauti kuhusu namna nchi yetu inavyopaswa kuendeshwa."
Seneta huyo aliongeza kuwa si yeye pekee anayekumbwa na vitisho kutokana na misimamo yake ya kisiasa. Alimtaja mwenzake wa Kaunti ya Vihiga, Seneta Godfrey Osotsi, ambaye alishambuliwa katika mkahawa alipokuwa akinywa chai.





















