Miaka 15 ya Sudan Kusini na Uchaguzi Mkuu unaosuburiwa kwa hamu
AFRIKA
3 dk kusoma
Miaka 15 ya Sudan Kusini na Uchaguzi Mkuu unaosuburiwa kwa hamuWengi wanaamini kuwa uchaguzi wa Disemba mwaka huu, utatoa fursa ya uundwaji wa serikali mpya itakayochochea uwajibikaji.
Kwa sasa, taifa hilo linajiandaa na uchaguzi mwezi Disemba 2026, licha ya wasiwasi uliotawala kuhusu mchakato huo./Picha:Wengine

Ni miaka 15 sasa tangu Sudan Kusini ijipatie uhuru wake kutoka Sudan.

Hata hivyo, taifa hilo changa zaidi duniani linaendelea kukabiliana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, huku uchaguzi nchini humo ukihairishwa mara nne.

Kwa sasa, taifa hilo linajiandaa na uchaguzi mwezi Disemba 2026, licha ya wasiwasi uliotawala kuhusu mchakato huo.

Haya, yanajiri pia wakati ambapo kuna msuguano kati ya Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake, Riek Machar.

Wawili hao walihusika na mkataba wa amani wa mwaka 2018, kufuatia vita vya mwaka 2013, vilivyogharimu maisha ya watu wapatao 400,000.

Wengi wanaamini kuwa uchaguzi wa Disemba mwaka huu, utatoa fursa ya uundwaji wa serikali mpya itakayochochea uwajibikaji.

“Tunataka twende zaidi ya mkataba ule wa amani. Ni kupitia chaguzi tu, ndipo tutaweza kutengeneza serikali halali na zenye uwajibikaji,” anasema Profesa Abraham Kuol Nyuon, mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Juba, katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Maeneo mengi ya nchi hiyo yamekumbwa na vurugu, huku raia wengi wakiyakimbia makazi yao.

Kikundi cha SPLM-IO, kinachoongozwa na Machar, kimetahadharisha kuhusu uandikishwaji wa wapiga kura na kuendesha kampeni kwenye maeneo yanayodhibitiwa na kikundi hicho, kikisitiza kuwa, “nchi hiyo bado iko vitani”.

Kwa mara kadhaa sasa, chaguzi za Sudan Kusini zimekuwa zikisogezwa mbele.

Hapo awali, mchakato huo ulipangwa kufanyika mwaka 2015, 2018, 2021, 2023, na mwishoni mwa mwaka 2024.

Licha ya kutenga Disemba 22, 2026 kama siku ya uchaguzi, mashirika mbalimbali kama vile Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hatari nchini humo.

“Bila kuwepo na maridhiano, hatuwezi kuendelea na mchakato wa uchaguzi wa amani na utulivu,” anasema mwanaharakati wa haki za kibinadamu, Edmond Yakani.

Vikwazo vya kifedha na kisheria

Akitangaza siku ya uchaguzi, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya nchi hiyo Abednego Akok Kacuol, alikiri uwepo wa changamoto za kifedha na kisheria kabla ya mchakato huo.

Kulingana na mwenyekiti huyo, serikali ndio chanzo pekee cha upatikanaji wa fedha hizo.

Kati ya Dola milioni 250 zinazohitajika kuandaa uchaguzi huo, tume hiyo imepokea Dola milioni 21, huku 15 zikitoka kwa wadau wa kimataifa, huku 6 zikitolewa na serikali.

“Kuna changamoto nyingi zenye kuathiri tume hiyo, tunaiomba serikali iweze kuzitatua ndani ya muda mfupi,” alieleza.

Wiki iliyopita, serikali ya nchi hiyo, ilitatua baadhi ya changamoto za kisheria kwa kuidhinisha baadhi ya kanuni za amani kuelekea hadidu za rejea za uchaguzi.

Kulingana na serikali ya nchi hiyo, uamuzi huo unalenga kusukuma mbele matayarisho ya uchaguzi.

Hata hivyo, wachunguzi wa mambo wanaamini kuwa uwezo wa kukabiliana na changamoto hizo upo kwa Rais  Kiir na serikali yake nzima.

Katika taarifa yake iliyotolewa mwezi uliopita, ofisi ya rais wa Sudan Kusini ilisema kuwa itahakikisha kuwa nchi hiyo inatimiza wajibu wake wa kidemokrasia.

Kulingana na Kiir, majadiliano ndani ya chama kuhusu mchakato mzima, yalikuwa yakiendelea.

Mwezi uliopita, Mwakilishi Mkuu wa Eneo la Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu Jakaya Kikwete, alikutana na Rais Kiir na kusifu juhudi za kusajili vyama vya siasa, kuendesha elimu ya uraia na kuandaa katiba mpya.

Wachambuzi wanasema uchaguzi ni muhimu kwa Sudan Kusini katika kuimarisha demokrasia na ushiriki wa kisiasa wa raia pamoja na kuleta utulivu katika taasisi za serikali.

Hata hivyo, baadhi ya waangalizi bado wana shaka kuhusu utayari wa uchaguzi.

"Ndiyo tunahitaji uchaguzi, ndiyo ni wito maarufu kutoka kwa raia, ndiyo ni mchakato mzuri wa kukomesha kipindi cha mpito, lakini tunahitaji kuwa na uchaguzi ambao haurudishi nchi vitani," anasema Yakani.

CHANZO:TRT Afrika