Mkuu wa jeshi la Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba ameamuru kufungwa kwa vyombo viwili vikubwa vya habari nchini humo.
Kainerugaba, ambaye pia ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni na anatazamwa na watu wengi kama mrithi anayetarajiwa, alitangaza kwenye X kwamba aliamuru kufungiwa kwa gazeti la Daily Monitor na NTV Uganda, akisema "haamini katika vyombo vya habari huru" na kwamba vyombo vya habari vinapaswa "kuongozwa na makada wa mapinduzi."
Hakutoa sababu ya agizo hilo. Wanajeshi baadaye walitumwa katika majengo ya Nation Media Group (NMG) mjini Kampala, na kuzuia wafanyakazi kuingia au kutoka, huku televisheni na redio zikifungiwa kurusha matangazo hewani.
Hatua hiyo ni ya hivi punde zaidi katika uhusiano wa Kainerugaba ambao mara nyingi humgonganisha na wanahabari.
Katika miaka ya hivi karibuni, jenerali huyo ametumia mara kwa mara akaunti yake ya X kukosoa waandishi wa habari, na mashirika ya vyombo vya habari, akijipatia jina la utani "mkuu wa tweeting" kwa machapisho yake ya uchochezi na mara nyingi ya utata.
Matamshi yake ya mtandaoni mara kwa mara yamezua vichwa vya habari na mabishano ya kidiplomasia, ikiwa ni pamoja na maoni yanayolenga viongozi wa upinzani na serikali za kigeni.
Mapema kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, mamlaka ilipiga marufuku matangazo ya moja kwa moja ya ghasia na matukio ya vurugu na baadaye kuamuru kufungwa kwa mtandao, ikisema kuwa hatua hizo ni muhimu ili kupambana na habari potofu na kulinda usalama wa taifa, maamuzi ambayo yalileta ukosoaji kutoka kwa vikundi vya haki na watetezi wa uhuru wa vyombo vya habari.
Magazeti ya Daily Monitor na NTV Uganda yanamilikiwa na Nation Media Group yenye makao yake nchini Kenya, mojawapo ya makampuni makubwa zaidi ya habari ya Afrika Mashariki.
Serikali ya Uganda na NMG wote hawajatoa maoni juu ya kufungwa kwa mashirika hayo Jumapili.

















