Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Sudan Abdel Fattah al-Burhan ataongoza ujumbe kuelekea Kongamano la tatu la Urusi na Afrika jijini Moscow Oktoba 28 na 29, shirika la habari la taifa SUNA liliripoti siku ya Jumanne.
Ujumbe huo utajumuisha mawaziri wa mambo ya nje na fedha, mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi na Mkuu wa Viwanda vya Mifumo ya Kijeshi.
Burhan anatarajiwa kuhutubia mkutano huo, kufanya mazungumzo ya pamoja na Rais wa Urusi Vladimir Putin na kutembelea Chuo Kikuu cha Urusi.
Balozi wa Sudan nchini Urusi Mohamed al-Ghazali al-Tijani Siraj amesema ziara hiyo inakuja huku ushirikiano kati ya Sudan na Urusi ukiimarika, hasa katika majukwaa ya kimataifa.
Amesema Urusi inaweza kuwa na nafasi muhimu katika ujenzi upya wa Sudan, hasa kwenye sekta ya nishati, mafuta, madini, kilimo, miundombinu na elimu ya juu.
Balozi huyo pia alieleza kuwa nchi hizo mbili zinaadhimisha miaka 70 ya uhusiano wa kidiplomasia mwaka huu.
Kulingana na Siraj, zaidi ya viongozi wa nchi na serikali 36 wamethibitisha ushiriki wao katika kongamano hilo.
Mkutano huo unatarajiwa kujadili ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi, ikiwemo mpango wa ushirikiano kati ya Urusi na Afrika wa 2027-2029 na ushirikiano kuhusu masuala ya akili mnemba.
Sudan imekuwa na mapigano kati ya jeshi na wapiganaji wa RSF tangu Aprili 2023, kusababisha vifo vya maelfu ya watu na mamilioni kuondoka katika makazi yao.
Mapigano hayo yameharibu miundombinu ya nchi na kusababisha hali mbaya zaidi kwa watu kuwahi kutokea duniani, kukiwa na ukosefu wa chakula na ukame katika maeneo kadhaa.


















