| Swahili
UTURUKI
3 dk kusoma
Ukiukaji wa Israel huko Gaza unadhoofisha imani katika mfumo wa kimataifa: Fidan
Hakan Fidan ataka kuruhusiwa kwa misaada ya kibinadamu, kulindwa kwa watoto na kupatikana kwa suluhisho la kisiasa la haki, huku akieleza mkakati wa Uturuki wa upatanishi katika mkutano uliofanyika Istanbul.
Ukiukaji wa Israel huko Gaza unadhoofisha imani katika mfumo wa kimataifa: Fidan
Fidan alisema kuwa juhudi za upatanishi za Uturuki zinategemea ridhaa ya pande husika, kuaminiana, na ushirikishwaji. /

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, amesema kuwa ukiukaji wa kila siku unaofanywa na Israel dhidi ya makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza unadhoofisha imani katika mfumo wa kimataifa na kuchochea hali ya kutokuaminiana.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Tisa wa Istanbul kuhusu Upatanishi, uliofanyika Ijumaa, Fidan amesema kuwa ukaliaji wa ardhi unaendelea Gaza na katika Ukingo wa Magharibi, huku vitendo hivyo vikifanyika bila wahusika kuwajibishwa.

Amisisitiza kuwa kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia wahitaji na kuhakikisha ulinzi wa watoto, hususan, ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele. Pia amesisitiza kuwa mzozo wa Israel na Palestina unaweza kutatuliwa tu kupitia suluhisho la kisiasa la haki.

Mazungumzo na kuaminiana

Fidan amesema juhudi za Uturuki katika upatanishi zinategemea ridhaa ya pande zinazohusika, kuaminiana na ushirikishwaji wa wote, akitolea mfano juhudi za Uturuki nchini Libya.

“Juhudi za Uturuki nchini Libya, kwa mfano, zinaonesha jinsi ridhaa, kuaminiana na ushirikishwaji wa wote vinavyoweza kujenga imani,” amesema.

Ameongeza kuwa Uturuki inashiriki katika mazungumzo yanayolenga kuzaa matunda nchini Libya na pande zote, za Magharibi na Mashariki, pamoja na washirka wa kimataifa.

Kwa mujibu wa Fidan, mchakato unaoongozwa na Walibya wenyewe na unaotegemea mazungumzo ya dhati ndiyo njia pekee ya kufikia suluhisho la kudumu nchini humo.

Amesisitiza kuwa njia za mawasiliano zinapaswa kubaki wazi hata pale maendeleo yanapokuwa ya polepole na yasiyo na uhakika.

Amesema mtazamo huo umeongoza juhudi za Uturuki katika mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine, mpango wa usafirishaji wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi, pamoja na mchakato wa Uturuki kati ya Somalia na Ethiopia.

Nchi za eneo husika kuamua maswala yao

Akizungumzia makubaliano ya hivi karibuni ya ulinzi yaliyosainiwa mjini Makkah kati ya Uturuki, Pakistan na Saudi Arabia, Fidan amesema muungano huo “unalenga kuhakikisha amani, ustawi na mustakabali wa eneo hilo.”

Ameeleza kuwa msingi wa makubaliano hayo, ambao ni nchi za eneo husika kuamua maswala yao, unaongeza uwezekano wa juhudi hizo kufanikiwa.

Aidha, ameitaja Jukwaa la Amani la Balkan kama utaratibu unaozingatia umiliki wa masuala ya kikanda na unaoweza kusaidia kugeuza mazungumzo kati ya mataifa ya Balkan kuwa vitendo.

Fidan alisisitiza kuwa Uturuki imefanya kazi mfululizo ili kuinua upatanishi kutoka kuwa chombo cha kidiplomasia na kuufanya kuwa taaluma ya kimkakati, na imejenga mfumo wa kitaasisi unaoendana na azma hiyo.

“Hatulazimishi suluhisho kwa pande husika, bali tunaunda mazingira ambayo yatawezesha pande zinazohusika kufikia suluhisho lao wenyewe,” amesema.

Amefafanua kuwa upatanishi hauhusu kuamua nani atashinda, nani atashindwa au nani atalegeza msimamo, bali ni kutafuta maridhiano na kufanya kazi kwa pamoja ili kufikia suluhisho ambalo linazinufaisha pande zote.

Fidan amehitimisha kwa kusema kuwa uzoefu wa Uturuki, unaotegemea mazungumzo ya dhati, ushirikishwaji endelevu na umiliki wa maswala ya kikanda, unaonesha jinsi mtazamo huo unavyoweza kuchangia usalama wa kikanda na wa kimataifa.

CHANZO:AA