Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anasema Uturuki itaendelea na juhudi zake za kidiplomasia na upatanishi kwa lengo la kutatua migogoro, na kuonya kuwa kupungua kwa uaminifu miongoni mwa taasisi za kimataifa kunazidisha ukosefu wa usalama duniani.
Katika ujumbe kwa njia ya video kwa Kongamano la 9 la Upatanishi la Istanbul, Erdogan alishkuru wizara ya mambo ya nje kwa kuandaa mkutano huo na kupongeza nafasi ya jiji la Istanbul kama kituo cha kidiplomasia.
“Nimefurahi kuwa Istanbul, ambayo kwa karne kadhaa imeleta watu na tamaduni mbalimbali pamoja, na sasa imekuwa moja ya kituo cha diplomasia,” alisema.
Erdogan alisisitiza umuhimu wa kuendeleza diplomasia huku migogoro ikizidi, uhasama ukiongezeka na imani ikipungua kwa sheria na taasisi za kimataifa.
“Kama Uturuki, tumesisitiza hili kuwa msimamo wetu hatutoachana na diplomasia, hata wakati pande tofauti zinapokataa kuzungumza na matumaini yanafifia,” alisema.
Alieleza kuachiwa huru kwa wafungwa kati ya Urusi na Ukraine na juhudi za upatanishi kote barani Afrika kama mifano ya kazi za Uturuki kufungua njia ya kupatikana kwa amani.
Erdogan alaumu ukosefu wa usawa duniani
Erdogan alisisitiza wito wake wa mabadiliko ya Umoja wa Mataifa, akirudia ujumbe wake wa “dunia ni kubwa kuliko mataifa matano” — kuashiria nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Alisema Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa uliokuwepo hivi karibuni chini ya mada “Kuimarisha Imani Tena”, ukilenga kurudisha imani katika mfumo wa kimataifa.
“Leo hii, mamilioni ya watu Palestina, Lebanon, Sudan na maeneo mengine yenye mizozo, ambao wameelekeza matumaini yao kwa Umoja wa Mataifa, na sasa wamekatishwa tamaa,” Erdogan alisema.
“Mfumo ambao utashi wa nchi zaidi ya 190 unategemea maamuzi ya mataifa matano siyo sahihi au wenye uwezo wa kurudisha imani kamili,” aliongeza.
Erdogan alisema Uturuki imekataa mtazamo wa siasa za kimataifa uliojengwa kwa msingi wa kutoaminiana na kusisitiza kuwa diplomasia inawezekana hata wakati wa mizozo mikubwa.
“Suala hilo ni kama tunaweza kuonesha utashi, ujasiri na uwazi wa kuendeleza hayo,” alisema, akiongeza kuwa Uturuki itaendelea kuleta pande tofauti pamoja, upatanishi kwa lengo la kupatikana kwa suluhu ya haki na kuwa msimamizi wa amani.























