| Swahili
AFRIKA
3 dk kusoma
Rais wa Shirikisho la Soka Nigera ajiuzulu kufuatia tuhuma za rushwa na matokeo mabovu
Ibrahim Musa Gusau amejiuzulu huku shinikizo likiongezeka dhidi ya Shirikisho la Soka la Nigeria kutokana na madai ya matumizi mabaya ya fedha na kushuka kwa kiwango cha soka la nchi hiyo kimataifa.
Rais wa Shirikisho la Soka Nigera ajiuzulu kufuatia tuhuma za rushwa na matokeo mabovu
Gusau alitetea uongozi wake na kusema matatizo ya kifedha ya NFF yameathiriwa pia na hali ngumu ya uchumi wa Nigeria. Picha: IG/ibrahim_musagusau

Rais wa Shirikisho la Soka Nigeria (NFF), Ibrahim Musa Gusau, amejiuzulu kutoka kwenye nafasi yake huku shinikizo likiongezeka dhidi ya shirikisho hilo kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha pamoja na matokeo mabovu ya timu za taifa katika mashindano ya kimataifa.

Gusau alitangaza kujiuzulu siku ya Alhamisi, Agosti 27, 2026, wakati NFF ikiwa inakabiliwa na ukosoaji mkubwa kufuatia kushindwa kwa timu za taifa kufuzu kushiriki kwa mashindano makubwa, ikiwemo Kombe la Dunia.

Uamuzi huo umefanyika takribani mwezi mmoja kabla ya uchaguzi mkuu wa NFF uliopangwa kufanyika Septemba 27 mjini Lafia, katika Jimbo la Nasarawa.

Katibu Mkuu wa NFF, Mohammed Sanusi, pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati kuu ya shirikisho hilo, pia wamejiuzulu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Abuja, Gusau alisema: “Nimeamua kujiuzulu kutoka nafasi yangu ya urais wa NFF,” na akaeleza kuwa aliwashauri pia wajumbe wengine wa bodi kujiuzulu.

Vyombo vya habari vya Nigeria vimeripoti kuwa NFF inachunguzwa na Idara ya Huduma za Usalama ya Nigeria (DSS) kuhusu madai ya matumizi mabaya ya Naira bilioni 17, sawa na takribani Dola milioni 12.7, ambazo shirikisho lilipokea kutoka kwa serikali mwaka 2024.

Fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya fedha zilizokuwa zikidaiwa na wachezaji na viongozi wa timu za taifa. Tuhuma hizo zimeongeza shinikizo kwa uongozi wa NFF wakati shirikisho hilo likikabiliwa pia na maswali kuhusu usimamizi wa idara yake.

Matatizo ya muda mrefu ya soka la Nigeria

Nigeria ni miongoni mwa mataifa yenye historia kubwa katika soka barani Afrika, lakini NFF imekuwa ikikabiliwa kwa muda mrefu na tuhuma za usimamizi mbaya na matatizo ya kifedha.

Wachezaji na makocha wa timu za taifa wamewahi kulalamika hadharani kuhusu kuchelewa au kutolipwa posho na fedha nyingine wanazodai.

Katika kipindi cha hivi karibuni, hali hiyo imezidi kuwa mbaya baada ya timu za taifa kushindwa kufuzu kwa mashindano muhimu.

Timu ya taifa ya wanaume, Super Eagles, ilishindwa kufuzu kushiriki katika michuano ya Kombe la Dunia la 2026 baada ya kupoteza kwa penalti dhidi ya timu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mchezo wa mchujo.

Kwa upande wa wanawake, Super Falcons walishindwa kufuzu kushiriki katika Kombe la Dunia la Wanawake la 2027 baada ya kufungwa 2-1 na Afrika Kusini katika mchezo wa mchujo. Na hivyo kufanya timu hiyo ya wanawake kutofuzu kushiriki katika Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mashindano hayo yaanze mwaka 1991.

Super Falcons ni mabingwa wa soka la wanawake barani Afrika, wakiwa wameshinda Kombe la AFCON mara 10. Hata hivyo kushindwa kufuzu kwao kwa mashindano ya mwaka 2027 kumekuwa pigo kubwa kwa soka la Nigeria.

Gusau ajitetea

Licha ya kujiuzulu, Gusau alitetea uongozi wake na kusema matatizo ya kifedha ya NFF yameathiriwa pia na hali ngumu ya uchumi wa Nigeria pamoja na mabadiliko ya thamani ya fedha za kigeni.

Pia alitangaza ushirikiano kati ya NFF na kampuni ya Adidas, ambao utaipa Nigeria malipo ya fedha taslimu ya dola milioni 4.5 kila mwaka.

CHANZO:AFP