| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Zambia yasema matamshi ya balozi wa Marekani anayeondoka 'si ya kidiplomasia'
Zambia inasema imeshangazwa na matamshi ya Balozi wa Marekani anayeondoka Michael Gonzales, ikiyataja kama yasiyo ya kistaarabu, yasiyo ya kidiplomasia na kinyume na utaratibu wa kuheshimiana.
Zambia yasema matamshi ya balozi wa Marekani anayeondoka 'si ya kidiplomasia'
Zambia inasema matamshi ya Balozi wa Marekani anayeondoka Michael Gonzales' si ya kidiplomasia. / Wengine

Siku ya Jumatatu Zambia ilieleza kushtushwa kwake na matamshi ya balozi wa Marekani anayeondoka Michael Gonzales, ikiyataja kama yasiyo ya kistaarabu, yasiyo ya kidiplomasia na kinyume na utaratibu wa kuheshimiana, kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje.

Akizungumza mjini Lusaka siku ya Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Nje Mulambo Haimbe alisema matamshi ya balozi huyo, aliyoyasema wakati wa hafla ya kumuaga wiki iliopita, hayakutolewa kwa njia rasmi za kidiplomasia, jambo ambalo anasema ni kutoheshimu utaratibu uliopo.

Amesema kutokuwepo kwa malalamiko rasmi au sera maalum kunaonesha “ukosefu wa heshima” kwa Zambia.

"Kwa hiyo Serikali ya Zambia inashtumu muenendo wa balozi anayeondoka. Tunatoa wito kwa raia wote wa Zambia na washirika wa kimataifa kupuuza matamshi yaliyotolewa na balozi anayeondoka wakati wa hafla iliyoandaliwa kwa ajili ya kumuaga," Haimbe alisema.

Ushirikiano wa Zambia, Marekani haufungamanishwi na misaada, Zambia inasema

Katika karamu hiyo siku ya Alhamisi mjini Lusaka, Gonzales alieleza wasiwasi wake kuhusu juhudi za Zambia za kupambana na ufisadi na masuala ya mifumo ambayo yanahusishwa na misaada katika sekta ya afya, kulingana na maafisa.

Haimbe alikanusha madai kuwa, uhusiano wa Zambia na Marekani haufungamanishwi na misaada, bali ni ushirikiano thabiti ambao msingi wake ni wa kimkakati.

"Ushirikiano huu umekuwa na tija kwa raia wa nchi zote mbili tangu ulipoanza na hauwezi kufungamanishwa na misaada kama ilivyoelezwa na balozi anayeondoka. Kufanya hivyo ni dharau kubwa kwa mababu zetu ambao walikuwa na ndoto ya urafiki wa mataifa mawili, ambayo pamoja na kuwa tofauti kimaendeleo, yana lengo moja, la msingi wa usawa kwa mataifa yote," aliongeza.

Alisema Zambia bado ni taifa huru ambalo sheria zake na taasisi zake lazima ziheshimiwe, na kuonya kuhusu taarifa za kudunisha utawala bora wa nchi hiyo au uongozi wake.

Zambia 'iko tayari kwa ushirikiano wenye tija'

"Serikali iko tayari na ina dhamira ya kuimarisha misingi ya utawala bora, kupambana na ufisadi na kufikisha maendeleo endelevu kwa wananchi kulingana na vipaumbele vya taifa.

"Kwa sasa, Zambia iko tayari kwa ushirikiano wenye tija na washirika wake wote wa kimataifa kwa misingi ya sheria ya kimataifa na utaratibu uliopo wa kidiplomasia," waziri alisema.

CHANZO:AA