Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imepiga marufuku mikusanyiko mikubwa katika mji mku wa Kinshasa, na mikoa mingine mitatu katika juhudi za kudhibiti kuenea kwa virusi vya Ebola; Wizara ya Mambo ya Ndani imesema katika agizo lilotolewa kwa magavana wa mikoa hiyo siku ya Jumapili.
Mikutano ya kisiasa, maandamano, na mikusanyiko mingine ambayo inaweza kuvutia umati mkubwa imepigwa marufuku katika majimbo ya Kinshasa, Tshopo, Haut-Uele na Bas-Uele, kulingana na agizo lililotiwa saini na Waziri wa Mambo ya Ndani Jacquemain Shabani.
Mlipuko wa Ebola umejikita zaidi katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Serikali imesema hatua hiyo inalenga kuzuia ugonjwa huo kusambaa hadi maeneo jirani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya iliyotolewa Jumatatu, idadi ya maambukizi ya Ebola iliyothibitishwa imefikia 1,274, huku watu 360 wakifariki dunia tangu mlipuko huo ulipotangazwa rasmi Mei 15, 2026.
Hatua hizi mpya zimefuatia utekelezaji wa karantini ya lazima ya siku 21 kwa wasafiri wanaotoka katika maeneo yaliyoathiriwa na Ebola.
Mwezi uliopita, viongozi pia walisimamisha michezo na shughuli zingine za kijamii huko Ituri, kitovu cha mlipuko huo.

















