Bara la Afrika linaweza kutumia mfano na uzoefu wa Togo, iwapo linataka kukabiliana na magonjwa yasiyopewa kipaumbele.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), ni kundi la magonjwa yanayoathiri mamilioni ya watu, hasa maeneo yenye umaskini na ukosefu wa maji safi.
Yamepewa jina hilo kwa sababu za kihistoria, ambapo yamekuwa hayapewi kipaumbele, licha ya kuathiri watu wapatao bilioni 1.5 ulimwenguni.
Togo yaonesha mfano
Ilipofika mwaka 2022, Togo ilikuwa ni nchi ya kwanza barani Afrika, kati ya nyingine nne, kufanikiwa kutokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele.
Magonjwa hayo ni kama vile minyoo, ugonjwa wa kusinzia pamoja na trachoma.
Licha ya mafanikio hayo, Togo imeendelea na harakati hizo, ikijiwekea malengo ya kutokomeza kabisa magonjwa mengine ikiwemo ukoma, ikifika mwaka 2030.
Katika taarifa yake, wizara ya nchi hiyo ilionesha nia dhabiti ya kutokomeza magonjwa hayo.
“Togo imeonesha uongozi pamoja na kutekeleza mikakati waliojiwekea,” anasema Dkt. Elizabeth Juma, kutoka katika taasisi ya WHO yenye kushughulikia magonjwa yasiyopewa kipaumbele.
Mapema mwaka huu, mataifa 22 barani Afrika yalifanikiwa kutokomeza walau ugonjwa mmoja usiopewa kipaumbele.
Kulingana na wataalamu wa afya, Afrika haijapoteza mwelekeo kuifikia shabaha hii.
“Kwa bahati mbaya, hatutofikia malengo ya mwaka 2030,” anaeleza Dkt. Juma.
Changamoto kubwa hapa ni utegemezi wa fedha kutoka kwa wahisani.
Hali ilizidi kuwa mbaya mara baada ya wahisani hao kujiondoa, hususani wakati wa janga la UVIKO-19.
Wataalamu hao, pia wamepigia chapuo suala la kutumia uwepo wa taasisi za utafiti za ndani.
“Baadhi ya serikali duniani zimeamua kukatisha fedha kwa ajili ya tafiti,” anasema Profesa Nicki Tiffin, Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kibaiolojia ya Afrika Kusini.
Mawazo hayo yanaungwa mkono na mtaalamu wa uzalishaji madawa kutoka Nigeria, Profesa Iruka Okeke.
“Tumekuwa tukipoteza vipaji vya wanasayansi wanaochipukia nchini Nigeria, kwa kiwango cha kushtua”, anasema Okeke katika mahojiano yake na TRT Afrika.
Hata hivyo, kulingana na Dkt. Juma, baadhi ya mataifa ya Afrika, yameanza kuchukua mfumo huu.
Kuwekuwa na maboresho kwenye mifumo ya afya katika maeneo mbalimbali barani Afrika, kama vile Tanzania, Uganda na Madagascar.
















