Waziri wa zamani wa Uingereza, Sir Alan Duncan, alikuwa mwanasiasa wa kwanza kutoka Ulaya kutembelea Uturuki baada ya jaribio la mapinduzi la Julai 15, 2016 lililopangwa na Shirika la Kigaidi la Fetullah (FETO), alisema ilikuwa muhimu kufika nchini humo ili kuonesha wazi kwamba Uingereza ilisimama upande wa serikali iliyochaguliwa kidemokrasia.
Akikumbuka matukio ya Julai 15, Duncan alisema alipata taarifa za jaribio la mapinduzi katika siku yake ya kwanza kabisa kuanza kazi serikalini. Baada ya kuzungumza na aliyekuwa Balozi wa Uingereza nchini Uturuki wakati huo, Richard Moore, aliamua mara moja kusafiri kwenda Ankara ili kuonesha mshikamano na taifa hilo.
Duncan alisema kuwa kwa mara ya kwanza alisikia kuhusu jaribio la mapinduzi jioni ya tarehe 15 Julai 2016, mara tu baada ya serikali mpya ya Uingereza kuundwa chini ya Waziri Mkuu wa wakati huo, Theresa May, na katika siku yake ya kwanza kuhudumu kama Waziri wa Nchi katika Wizara ya Mambo ya Nje.
Alisema alipofika ofisini jioni ya Julai 15, 2016, katibu wake alimfahamisha kuwa kulikuwa na jaribio la mapinduzi nchini Uturuki. Waliwasha televisheni na kufuatilia taarifa za habari kuhusu ndege za kijeshi zilizokuwa zikipaa nchini humo na hali ilivyokuwa ikiendelea.
"Tulipata taarifa zote na nikasema, 'Nataka kuzungumza na balozi kupitia njia ya simu.' Wengine waliona hilo si jambo la kawaida kwa waziri mpya, lakini nikasema, 'Hapana, namtaka balozi. Sihitaji mtu mwingine aniambie nifanye nini”, Duncan alikumbuka tukio hilo.
Baada ya kuzungumza na Richard Moore na kupata maelezo kuhusu hali ilivyokuwa, Duncan alisema alimwambia: "Nitakuja kutembelea Uturuki."
Moore alimkaribisha, lakini akamuuliza kama angependa kusubiri ushauri kutoka Wizara ya Mambo ya Nje. Duncan alisema alimjibu: "Hapana. Mimi ndiye waziri. Ninakuja."
Kwa mujibu wa Duncan, hakukuwa na mtu serikalini London ambaye angeweza kuzuia safari hiyo, kwani serikali mpya ilikuwa bado inaendelea kujipanga. Hivyo alichukua uamuzi binafsi na kusafiri kwenda Ankara.
"Ilikuwa muhimu sana"
Duncan alisema alikuwa waziri wa kwanza kutoka Ulaya kutembelea Uturuki baada ya jaribio hilo la mapinduzi. Alibainisha kuwa baadhi ya nchi za Ulaya zilichelewa kutoa msimamo wao, huku wengine wakidai kwamba lilikuwa tukio la kuigiza.
"Baadhi yao walikuwa wakisema, 'Haya ni mapinduzi ya kuigiza, si ya kweli.'"
Hata hivyo, alisema yeye hakuwahi kuwa na shaka kwamba jaribio hilo lilikuwa la kweli.
"Ilikuwa muhimu sana kwenda na kusema kwamba huwezi kuiondoa serikali iliyochaguliwa kwa kutumia vurugu, uasi au mapinduzi. Serikali iliyochaguliwa lazima iheshimiwe na kuungwa mkono."
Alisisitiza kuwa msimamo wake ulikuwa wazi: "Ilikuwa muhimu kuunga mkono demokrasia ya Uturuki na kuonesha wazi kwamba huo ndio ulikuwa msimamo wa Uingereza."
Aidha alisema alitaka pia kuhakikisha wafanyakazi wa Ubalozi wa Uingereza jijini Ankara walikuwa salama, lakini ujumbe mkuu ulikuwa kuunga mkono demokrasia ya Uturuki.
Duncan alisema kutembelea Bunge Kuu la Taifa la Uturuki baada ya mashambulizi kulimwathiri sana.
"Unaweza kuona picha kwenye televisheni, lakini unapofika eneo lenyewe na kuona vifusi, vyuma vilivyopinda na vioo vilivyovunjika, ndipo unatambua ukubwa wa tukio."
Aliongeza kuwa shambulio hilo halikulenga jengo pekee bali lilikuwa shambulio dhidi ya taasisi ya demokrasia. "Hili si jengo tu. Hili ni Bunge, na Bunge ndilo moyo wa mfumo wowote wa kidemokrasia."
"Hili halikubaliki"
Ili kuwaeleza Waingereza uzito wa tukio hilo, Duncan alisema alilinganisha jaribio hilo na hali ambayo sehemu ya jeshi la Uingereza ingeasi, ikavusha mizinga kwenye Daraja la London Bridge, ikalishambulia Bunge wakati kikao kinaendelea, na kujaribu kumuua Waziri Mkuu pamoja na Malkia.
Alisema baadaye alitumia mfano huo ndani ya Bunge la Uingereza kwa sababu ulieleza kwa uwazi ukubwa wa kile ambacho Uturuki ilikabiliana nacho.
Duncan pia aliisifu jamii ya Uturuki kwa namna ilivyokabiliana na jaribio hilo la mapinduzi.
"Nilivutiwa sana na utulivu wao na namna walivyoshughulikia hali hiyo. Hakukuwa na ghasia kubwa."
Alisema wananchi walitoa ujumbe mmoja ulio wazi: "Hili halikubaliki. Tunaunga mkono demokrasia yetu, na wafuasi wa Guleni pamoja na wote waliojaribu kuipindua serikali hawakubaliki kwa wananchi wa Uturuki."
Aliongeza kuwa namna wananchi wa Uturuki walivyoungana kuilinda demokrasia yao ilikuwa jambo la kutia moyo sana.
Akikumbuka matukio hayo baada ya miaka kumi, Duncan alisema historia inapaswa kukumbuka kwamba jaribio hilo la mapinduzi lilishindwa na lilistahili kushindwa.
Kwa mtazamo wake, Uturuki imeimarika zaidi katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.
"Angalia kilichotokea ndani ya Uturuki katika miaka kumi iliyopita. Imekuwa nguvu muhimu zaidi katika kanda hio, imekuwa imara zaidi, imeimarisha uchumi wake na imepata ustawi mkubwa."
Alihitimisha kwa kusema: "Natumaini katika miongo mingi ijayo, Uturuki itaendelea kupata mafanikio kama haya."



















