Watu wasiopungua watano wauawa na wengine 16 wajeruhiwa kufuatia mlipuko wa bomu uliotokea katika mkahawa ulioko katikati ya jiji la Damascus, nchini Syria, kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Afya ya nchi hiyo iliyonukuliwa na kituo cha televisheni cha Alikhbariah.
Mlipuko huo ulitokea siku ya Alhamisi ulisababishwa na kilipuzi kilichokuwa kimefichwa ndani ya mkahawa huo.
Televisheni ya taifa ilisema, "Mlipuko uliotokea katika mkahawa uliopo karibu na Jengo la Mahakama Kuu jijini Damascus ulitokana na kilipuzi kilichokuwa kimewekwa katika eneo hilo." Mamlaka zaendelewa na uchunguzi kubaini chanzo cha mlipuko huo.
Kabla ya hapo, Alikhbariah TV iliripoti kuwa mlipuko ulitokea ndani ya mkahawa ulioko Barabara ya Al-Nasr.
Wahudumu wa afya pamoja na vikosi vya usalama walionekana katika eneo la tukio kwenye barabara inayoelekea Soko la Kihistoria la Hamidiyeh, ambalo ni mojawapo ya maeneo yenye shughuli nyingi zaidi jijini Damascus.
Magari ya kusafirisha wagonjwa yalionekana yakipenya kwenye msongamano wa magari huku ving'ora vikilia kwa kasi yakielekea eneo la tukio, wakati vikosi vya usalama vilizingira eneo lililotokea mlipuko.
Nour Khayyat (40), mmiliki wa duka la kuuza betri za mifumo ya nishati ya jua lililo karibu na eneo la mlipuko, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa, "Majira ya saa 6:00 mchana kwa saa za GMT, nilisikia mlipuko mkubwa na vioo vya duka langu vilitetemeka."
Aliongeza kuwa, "Watu walikimbilia kwenye mkahawa huo na kupiga simu kuomba huduma za ambulansi."
Mohammed al-Zahabi, mmiliki wa duka la miwani lililo jirani na mkahawa uliolengwa, alisema kwa sauti ya kutetemeka, "Baada ya mlipuko nilihisi msukumo mkubwa na eneo lote lilitikisika."
"Nilikimbilia eneo la tukio na nikawakuta watu wakiwa wamelala chini, damu ikiwa imetapakaa kila mahali," aliongeza.












