Maporomoko ya ardhi kusini mwa Tanzania yaliyosababishwa na mvua kubwa yameua takriban watu 20, hii ni kwa mujibu wa mamlaka za nchi hiyo, huku idadi ikitarajiwa kuongozeka.
Nchi za Afrika Mashariki zimekumbwa na mvua kali na kuleta mafuriko yaliyosababisha vifo vya watu 81 nchini Kenya huku makazi ya maelfu yakiharibiwa.
Nchini Tanzania, mvua kubwa zilizoambatana na upepo mkali zimesababisha maporomoko ya ardhi yaliyoharibu nyumba kadhaa mwanzoni siku ya Jumatano huko mkoani Mbeya, amesema Jaffar Haniu, mkuu wa wilaya ya Rungwe ambapo maafa hayo yametokea.
"Idadi ya vifo imefikia 20," aliwaambia waandishi wa habari, na kuongeza kuwa miili 18 imepatikana Jumatano na miwili ilipatikana siku ya Alhamisi.
Mvua zaidi zinatarajiwa
"Mmoja wa waathiriki ni mtoto mdogo, mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu," aliongeza Haniu, huku akiwataka wananchi "kuchukua tahadhari" wakati mvua zaidi zikitegemewa.
Amewataka wale walio katika maeneo hatarishi kuondoka.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imetabiri mvua zaidi katika maeneo mbalimbali ya nchi hadi kufikia Jumanne wiki ijayo.










