| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Traoré wa Burkina Faso aonya dhidi ya kulinganishwa na Thomas Sankara
Kapteni Ibrahim Traoré amesema si sahihi kumlinganisha na aliyekuwa rais wa Burkina Faso, Thomas Sankara, akieleza kuwa mazingira ya kisiasa na kijamii ya sasa ni tofauti kabisa na yale ya miaka ya 1980.
Traoré wa Burkina Faso aonya dhidi ya kulinganishwa na Thomas Sankara
Kiongozi wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré (kushoto), amekuwa akifananishwa mara kwa mara na Thomas Sankara. /

Kiongozi wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, ametoa tahadhari dhidi ya kulinganishwa na Thomas Sankara, aliyekuwa rais wa nchi hiyo, ambaye aliuawa mwaka 1987.

Traoré, aliyeingia madarakani mwaka 2022 akiwa na ajenda ya kupigania umoja wa Afrika na kupinga ukoloni mamboleo, alisema huenda asitokee "Thomas Sankara mpya" katika kipindi hiki kwa sababu mazingira ya kisiasa na kijamii yamebadilika kwa kiasi kikubwa tangu miaka ya 1980.

Ametoa kauli hiyo siku ya Alhamisi wakati wa mazungumzo na wadau katika eneo la Yaadga.

"Hakuna makapteni wawili ndani ya mashua moja. Kwa hiyo epukeni kufanya kosa la kuwachanganya. Hakuna namba moja, hakuna namba mbili, wala namba gani?" alisema Traoré.

Thomas Sankara, anayejulikana kama "Baba wa Mapinduzi ya Burkina Faso", aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1983 yaliyofanywa kwa ushirikiano na mwenzake Blaise Compaoré.

Aliongoza nchi hiyo hadi alipouawa mwezi Oktoba mwaka 1987.

Sankara anakumbukwa kwa kutekeleza sera na mageuzi ya kijamii na kiuchumi yaliyokuwa ya maendeleo, ambayo yaliboresha maisha ya wananchi wengi wa Burkina Faso.

"Mazingira tunayoishi leo si yale ya miaka ya 1980. Tuwe wazi, mimi sikuwa gerezani halafu mtu akaja kunitoa gerezani baada ya mapinduzi ya kijeshi ili aniweke madarakani, kama ilivyokuwa kwa Blaise na Sankara. Hali ni tofauti kabisa," Traoré aliongeza.

Traoré mwenye umri wa miaka 38 kwa sasa ndiye kiongozi wa nchi mwenye umri mdogo zaidi duniani, na mtindo wake wa uongozi pamoja na falsafa yake ya kisiasa mara nyingi hulinganishwa na ule wa Thomas Sankara.

CHANZO:TRT Afrika