Mwamuzi wa Somalia Omar Abdulkadir Artan, ambae hakuruhusiwa kuingia nchini Marekani kwa ajili ya kuendesha mechi ya Kombe la Dunia 2026, amerudi nchini mwake siku ya Jumanne akitokea Istanbul.
Artan amesema "ndoto kubwa ya maisha yake" imekatishwa baada ya kurudishwa kutoka Uwanja wa Ndege wa Marekani.
"Nimesikitishwa sana," Artan aliiambia The New York Times kutoka Istanbul, ambapo alirudi baada ya kukataliwa kuingia Miami.
"Mimi ni mwamuzi tu ninayejaribu kuishi ndoto yangu, ndoto kubwa ya maisha yangu, kuja katika Kombe la Dunia."
Artan amesema alihojiwa na maafisa wa uhamiaji kwa saa 11 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami na baadae kupelekwa seli ambapo pia alishikiliwa kwa saa kadhaa kabla ya kurudishwa Uturuki.
"Nilikuwa na nyaraka zangu sahihi na kila kitu. Nilikuwa na viza sahihi," amesema.
Refa wa mwaka
Artan, ambae mwaka 2025 alitajwa kama refa bora upande wa wanaume wa mwaka na Shirikisho la Soka Afrika, angekuwa refa wa kwanza kutoka Somalia kuendesha mechi katika Kombe la Dunia.
Alizuiwa kuingia kufuatia "wasi wasi wa mwendeno wake," imesema idara ya Ushuru na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani katika taarifa yake bila kutoa ufafanuzi zaidi.
Artan alipewa viza ya kuingia nchini Marekani wiki iliyopita, kwa mujibu wa Ubalozi wa Somalia nchini Kenya ambao ndio uliofuatilia mchakato huo.
Hatua ya kumzuia kuhudhuria Kombe la Dunia afisa aliyechaguliwa na FIFA sio ya kawaida.
Artan alitakiwa kukutana na marefa wenzake katika mafunzo ya Kombe la Dunia mjini Miami.
Inasikitisha sana
"Nataka kuishukuru FIFA kwa kuniunga mkono muda wote and watu wa Somalia pia. Naishukuru FIFA na CAF pia. Hivyo ndivyo ninavyoweza kusema," Artan amewaambia waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Istanbul kabla ya kupanda ndege ya Shirika la Ndege la Uturuki kuelekea Somalia.
Kwa upande wake, Shirikisho la Soka la Somalia limeonesha kusikitishwa kwake baada ya Artan kuzuiwa kuingia nchini Marekani.
Shirikisho hilo limesema hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu uamuzi huo, lakini ilitaka kuwepo kwa hali ya utulivu mpaka pale taarifa kamili itakapotolewa.















