Jeshi la Polisi Tanzania limetoa onyo kali kwa mtu yeyote au kikundi kinachojihusisha na vitendo vya kuzuia mabasi na malori kuendelea na safari zao barabarani, kufuatia kile kinachoelezwa kuwa ni vuguvugu la mgomo wa madereva katika baadhi ya mikoa nchini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Septemba 29, 2026, jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Tanzania (CP), Awadh Juma, amesema ni kosa kisheria kumzuia dereva yeyote kutoa huduma au kufanya hujuma dhidi ya vyombo vya usafiri na abiria.
"Polisi wanaelekeza kuwa haitasita kuchukua hatua kali sana kwa mtu yeyote yule atakayebainika kuzuia gari... siyo kuzuia tu, hata kufanya kitu chochote ambacho ni kinyume cha sheria dhidi ya mabasi hayo au kufanya hujuma yeyote dhidi ya madereva," ameonya CP Awadh.
Aidha, aligusia taarifa zinazosambaa kuhusu mfumo wa alama (pointi) za leseni akisema bado haujaanza kutumika na kwamba wananchi na madereva wasiongozwe na propaganda mitandaoni, huku akiwahakikishia wamiliki na madereva kuwa usalama umeimarishwa na wawasilishe huduma zao bila hofu yoyote.
Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa linaendelea kufuatilia na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote anayevunja amri na kuingilia shughuli za usafirishaji nchini humo.





















