Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Petrobas Katambi amesema nchi hiyo ipo salama kuelekea mashindano ya AFCON yanayotarajiwa kufanyika mwaka 2027.
Kulingana na Katambi, Tanzania ni salama na imejipanga kuhakikisha hali inaendelea kuwa hivyo hivyo, tangu mwanzo hadi mwisho wa michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
“Kiusalama kwa upande wetu tuko vizuri zaidi,tumejipanga kulingana na shughuli kubwa inayokuja mbele yetu lakini tuendelee kusisitiza suala la usalama ni la pande zote na ni wajibu wetu sote kuhakikisha nchi inakua salama,” alisema Katambi.
Waziri huyo, ameongeza kuwa serikali ya Tanzania inaendelea kupata ushirikiano na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mwenzake wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi katika maandalizi ya mashindano hayo ambayo yanatarajiwa kuleta manufaa makubwa, ikiwemo kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali.
Hakikisho hilo linakuja wakati ambapo kuna wasiwasi wa hali ya utulivu wa kisiasa wakati wa mashindano hayo hasa kutokana na msuguano uliopo kati ya serikali na chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu, Oktoba 2025.
Mashindano ya AFCON 2027 yanaandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya, na Uganda.


















