| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Jeshi la Sudan ladhibiti maeneo kadhaa Kordofan Magharibi, wapiganaji wa RSF wakimbia
Mafanikio hayo ya kijeshi yanafuatia kutekwa kwa eneo la Al-Khuway na jeshi la Sudan siku ya Ijumaa.
Jeshi la Sudan ladhibiti maeneo kadhaa Kordofan Magharibi, wapiganaji wa RSF wakimbia
Mafanikio hayo ya kijeshi yanafuatia kutekwa kwa eneo la Al-Khuway na jeshi la Sudan siku ya Ijumaa. / / AA

Jeshi la Sudan, na vikosi washirika, wamechukua udhibiti wa maeneo matatu ya jimbo la West Kordofan, huku wapiganaji wa RSF wakikimbia, kwa mujibu wa vyanzo vya kijeshi vilivyonukuliwa na shirika la habari la Anadolu siku ya Jumanne.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, wanajeshi wameendesha operesheni za msako katika vijiji mbalimbali vya eneo la Al-Khuway, pamoja na maeneo yaliyoko kaskazini na mashariki mwa Al-Nuhud na Abu Zabad.

Wakati huohuo, Kamati ya Dharura ya Dar Hamar, ambayo ni taasisi ya ndani inayotoa msaada wa kibinadamu, imetoa wito wa kupelekwa kwa chakula, dawa na mahitaji mengine ya dharura katika eneo la Al-Khuway.

Kamati hiyo imesema jeshi limefanikiwa kurejesha udhibiti wa maeneo kadhaaa katika eneo hilo. Pia imezitaka mamlaka za jimbo na wafanyabiashara kuandaa na kutuma misafara ya magari yenye bidhaa muhimu ili kukidhi mahitaji ya wakazi.

Siku ya Jumatatu, msemaji wa vikosi maalumu vya operesheni vya jeshi la Sudan, Mohamed Didan, aliliambia shirika la habari la Anadolu kuwa wanajeshi walikuwa wameiteka Al-Saatat, eneo lililoko kaskazini-mashariki mwa Abu Zabad.

Didan alieleza kuwa eneo le Abu Zabad lina umuhimu mkubwa wa kimkakati kwa kuwa linaunganisha maeneo ya kaskazini na kusini mwa jimbo la Kordofan Magharibi.

Mafanikio hayo ya kijeshi yanafuatia kutekwa kwa eneo la Al-Khuway na jeshi la Sudan siku ya Ijumaa. Kwa mujibu wa maafisa wa Sudan, eneo hilo liko umbali wa takribani kilomita 100 kutoka Al-Nuhud.

Vita kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha RSF vilianza Aprili 2023 na vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za kikanda zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), takribani watu milioni 11.4 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na vita hivyo.

CHANZO:AA